Rais Kikwete (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
ELIMU(EDUCATION IN TANZANIA)
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa sera yetu ya kupanua
fursa ya elimu kwa Watanzania katika ngazi zote. Mwaka huu vijana wetu
wengi zaidi walijiunga na elimu ya msingi, sekondari, ufundi na elimu
ya juu. Hivi sasa tunaelekeza juhudi zetu zaidi katika kuongeza ubora
wa elimu. Kwa ajili hiyo, tumechukua hatua za makusudi za kupanua
mafunzo na ajira za walimu wa shule za msingi na sekondari. Kwa mfano,
mwaka huu walimu 24,621 wapya waliajiriwa kati yao 11,379 wa shule za msingi na 13,242 wa shule za sekondari. Januari, 2013 tunategemea kuajiri walimu 28,746 kati yao 14,606 wa shule za msingi na 14,060 watakuwa wa shule za sekondari.
Kwa sababu hiyo, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi umeendelea kuwa mzuri. Hivi sasa kwa shule za msingi uwiano umefikia 1:46 ukilinganisha na 1:56 mwaka 2005. Uwiano unaostahili ni 1:40. Kwa upande wa sekondari uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi hivi sasa ni 1:29 ukilinganisha na 1:20
unaostahili. Kutokana na upanuzi wa vyuo vya kufundisha walimu nchini,
bila ya shaka baada ya miaka mitatu hivi upungufu wa walimu wa shule za
msingi na sekondari haitakuwa kilio tena.
Ndugu Wananchi;
Upatikanaji wa vitabu nao unazidi kuwa bora. Hivi sasa uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi ni 1:3 kwa shule ya msingi na sekondari 1:3 ukilinganisha na 1:5 kwa shule za msingi na sekondari 1:4
mwaka 2009. Hata hivyo, tutaendelea kuongeza mgao wa fedha katika
bajeti ya elimu ili kuongeza upatikanaji wa vitabu na vifaa vingine vya
kusomea na kufundishia. Tunataka katika muda mfupi ujao uwiano uwe 1:1.
Kwa upande wa maabara za sayansi, tarehe 4 Novemba, 2012, nilipokuwa
kwenye ziara ya Mkoa wa Singida, nilitoa agizo la kutaka ndani ya miaka
miwili, kuanzia mwaka 2013, kila shule ya sekondari ya kata nchini iwe
na majengo ya maabara yaliyokamilika. Yawe pia yanatumika kwa maana ya
vifaa na mahitaji muhimu. Nimewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya
kuhakikisha kuwa agizo hili linatekelezwa kwa ukamilifu. Kuanzia sasa,
katika ziara zitakazofanywa Mikoani na mimi, Makamu wa Rais na Waziri
Mkuu tutapenda kupata taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wake.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa ufundishaji imedhihirika kwamba mkakati maalum
unahitajika kuboresha ufundishaji wa masomo ya hisabati, kiingereza na
sayansi katika shule za msingi na sekondari. Matokeo ya mitihani ya
darasa la saba na kidato cha nne kwa miaka mingi sasa yanathibitisha
haja hii. Sasa wakati umefika kwa suala hili kulipa uzito unaostahili.
Tutafanya hivyo kuanzia mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment