airtel

airtel

.

.

Thursday, January 9, 2014

WAZIRI MKUU AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA ALGERIA LEO


 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda akiwa katika kikao na Ujumbe kutoka  nchi ya Algeria wakiongozwa na Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria Mhe. Youcef Youfsi (wa kwanza kulia) walipomtembelea jana Ofisini kwake. Wa kwanza Kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Profesa Sospeter Muhongo. Wengine katika picha ni Watendaji wa Mashirika ya nishati na gasi ya Tanzania.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda  (katikati) katika picha ya Pamoja na Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria Mhe. Youcef Yousfi na  ujumbe wake ( wa pili kushoto mstari wa mbele), Wa pili kulia ni Waziri wa Nishati na Madini Mhe.profesa Sospeter Muhongo .
Na Asteria Muhozya
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Pinda amesema Tanzania itakuza uhusiano na ushirikiano na nchi ya Algeria kutokana na nchi hiyo kuwa mfano mzuri kwenye uwekezaji wa rasilimali asilia.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana wakati Waziri wa Nishati na Migodi wa Algeria Mhe. Youcef  Yousfi alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, Algeria ni moja ya nchi zilizopiga hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya nishati za gesi na umeme  kutokana  na kwamba sekta hiyo inachangia takribani asilimia 60 ya uchumi wa nchi hiyo hali ambayo inatoa fursa kwa Tanzania kujifunza na kuendeleza sekta hiyo kutoka kwao.

 “Ni fursa nzuri kwetu kujua namna wenzetu walivyoweza kufanikiwa na kuendelea kwa kutumia rasilimali hizo. Hali ambayo imefanya nchi hii kuwa mwalimu wa Mataifa mengine yanayochipukia katika kuwekeza katika rasilimali hizo”. Alisema.

Aidha Waziri Mkuu aliongoza kuwa, Algeria ni nchi ya mfano kwa Tanzania ikizingatiwa kuwa, imezisaidia nchi kadhaa za Falme za kiarabu zilizofanikiwa  katika sekta hiyo ikiwemo pia nchi ya Qatar.
Akiongelea kuhusu Serikali kumiliki uchumi kupitia sekta hizo kama ilivyo kwa Algeria, Waziri Mkuu alisema Serikali inataka kuona nchi hii inafanikiwa katika hilo.

“Serikali ya Algeria inasimamia asilimia 51 ya hisa katika sekta hizo kupitia kampuni za umma, na sisi tuna makampuni kama  Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ( TPDC), na  Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) hivyo tunataka kujifunza kwa wenzetu kuona namna gani vyombo vyetu vya umma vinavyoweza kufanya kazi kwa kuangalia mifano ya wenzetu na kukidhi matarajio ya wananchi.” Alisema.

Kuhusu kuendeleza rasilimali watu katika sekta hiyo, Waziri Mkuu kwanza ameishukuru Serikali ya Algeria kwa kuendelea kutoa msaada wa ufadhili kwa wanafunzi kusoma nchini humo, lakini zaidi hasa katika masomo ambayo ni maalumu katika sekta hiyo.
Aliongeza kuwa, ni funzo kwa Tanzania kuona namna gani Serikali itavitumia vyuo vilivyoko nchini kuzalisha wataalamu wa sekta za gesi,mafuta,umeme na madini.

Vilevile alisema kuwa anaamini wizara ya Nishati na Madini imejipanga vizuri kutekeleza mipango na hivyo ameitaka Wizara kuhakikisha wananchi wanapata matokeo ya haraka katika muda mfupi.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Migodi Algeria Mhe. Youcef Yousfi ameishauri Serikali kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kwa kuwa yanatarajia kuleta tija kwa Tanzania huku watanzania wenyewe wakiwa na utaalamu mkubwa katika sekta hiyo. “Tunataka kuisaidia Tanzania kujua namna bora ya kusambaza umeme na gesi, ndio maana tuko hapa alisema”, Waziri Yousfi.

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...