TANZANIA ZINDABAAA
Waziri Mkuu Mizengo Pinda
---
HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB),
WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUHITIMISHA
MKUTANO WA KUMI NA TANO WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAREHE 28 JUNI, 2014
UTANGULIZI
a) Masuala ya Jumla
Mheshimiwa Spika,
1. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi
wa Rehema kwa kutupatia uzima na afya hadi kufikia siku ya leo.
Tumekuwepo hapa kwa takriban miezi miwili ambapo tumeweza kupokea na
kujadili Taarifa za Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka
2013/2014 na Mwelekeo kwa mwaka 2014/2015 kwa Wizara mbalimbali na
hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2014/2015.
2. Napenda kutumia nafasi hii
ya awali kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi nzuri ya kutukuka
ambayo wameifanya kwa nidhamu na ufanisi mkubwa, hususan wakati wa
Mjadala wa Bajeti ya Serikali na Mafungu ya Wizara za Kisekta. Kipekee
niwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Bajeti chini ya Uongozi mahiri wa
Mheshimiwa Mtemi Andrew John Chenge, Mbunge wa Jimbo la Bariadi
Magharibi kwa kazi yao nzuri ya kuchambua Bajeti ya Serikali na Sheria
zinazoambatana na masuala ya Bajeti. Changamoto zilikuwa nyingi,
lakini kwa pamoja tumekubaliana na kuafikiana. Kazi kubwa
iliyoko mbele yetu ni kwenda kushirikiana na Wananchi katika utekelezaji
wa Bajeti hii ili kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa Spika,
3. Katika kipindi hiki tukiwa hapa Bungeni, yapo matukio ya
kusikitisha yaliyotokea ambapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walipoteza
Wapendwa wao. Aidha, yapo matukio ya Kitaifa yaliyosababisha kupoteza
maisha ya Ndugu, Jamaa na Marafiki. Napenda kutumia nafasi hii kuwapa
pole Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote waliofikwa na misiba na
majanga mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wote waliopotelewa na Ndugu,
Jamaa na Marafiki.
Mheshimiwa Spika,
4. Kipekee niwape pole ndugu, jamaa na marafiki waliopotelewa
na ndugu zao na wote waliopata majeraha wakati kulipotokea Mlipuko wa
Bomu pale Darajani, Zanzibar. Tukio hili la kusikitisha halipendezi kwa
Nchi yetu. Niwaombe Wananchi wote kwa umoja wetu tushirikiane kuwa
Walinzi katika maeneo yetu na kuwezesha kuwatambua mapema wale wote
wenye nia mbaya ya kuharibu amani na utulivu katika Taifa letu.
b) Shughuli za Bunge
Mheshimiwa Spika,
5. Katika Mkutano huu Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya
kufanya uchaguzi wa Wajumbe wa Wawakilishi kwenye Bodi za Taasisi,
Mabaraza na Tume za Bunge. Napenda nitumie nafasi hii kumpongeza
Mheshimiwa Dkt. Terezya Luoga Huvisa, Mbunge wa Viti Maalum kuwa Mjumbe
katika Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere;
Mheshimiwa
Goodluck Joseph Ole-Medeye, Mbunge wa Arumeru Magharibi kuwa Mwakilishi
wetu katika Bunge la Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kusini mwa Africa
(SADC-PF); Mheshimiwa Alphaxard Kangi Lugola, Mbunge wa Mwibara kuwa
Mjumbe katika Tume ya Utumishi wa Bunge; Mheshimiwa Henry Daffa
Shekifu, Mbunge wa Lushoto; Mheshimiwa Sylvester Massele, Mbunge wa
Dole; na Mheshimiwa Zainab Rashidi Kawawa, Mbunge wa Viti Maalum wote
kuwa Wajumbe katika Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Aidha,
nawapongeza Mheshimiwa Beatrice Matumbo Shelukindo, Mbunge wa Kilindi na
Mheshimiwa Dkt. Maua Abeid Daftari, Mbunge wa Viti Maalum kuwa Wajumbe
wa Baraza la Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi – Muhimbili; na mwisho
nimpongeze Mheshimiwa Rashid Mfutakamba, Mbunge wa Igalula kuwa Mjumbe
wa Bodi ya Utawala ya Chuo cha Ufundi Arusha. Tunaamini wote
waliochaguliwa watatuwakilisha vyema katika Taasisi hizo.
Mheshimiwa Spika, 6. Pamoja na kupokea, kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, jumla ya Maswali 321 ya Msingi na 879 ya Nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 37 ya Msingi na 30 ya Nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, 6. Pamoja na kupokea, kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, jumla ya Maswali 321 ya Msingi na 879 ya Nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Aidha, Maswali 37 ya Msingi na 30 ya Nyongeza yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
7. Nitumie fursa hii
kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuuliza Maswali ambayo
yalilenga katika kuwaletea Wananchi maendeleo katika Majimbo yetu na kwa
Taifa letu kwa ujumla. Vilevile, niwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri
wote ambao wamefanya kazi kubwa ya kuandaa majibu na maelezo ya ziada
katika kila Swali lililoulizwa.
c) Miswada, Maazimio na Kauli za Serikali
Mheshimiwa Spika,
8. Katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya
kujadili Miswada, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Miswada
iliyowasilishwa na Serikali na kukamilisha hatua zote ni Muswada wa
Sheria wa Fedha wa Mwaka 2014 [The Finance Bill 2014]; na Muswada wa
Sheria wa Kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2014 [The
Appropriation Bill, 2014].
Mheshimiwa Spika,
9. Miswada ifuatayo imesomwa kwa mara ya kwanza:
i) Muswada wa Sheria wa Kufanya
Marekebisho katika Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta
Binafsi wa 2014 [The Public Private Partnership (Amendment) Act, 2014]
ulisomwa kwa mara ya kwanza.
ii) Muswada wa Sheria ya Utawala wa Kodi 2014 (The Tax Administration Act 2014);
iii) Muswada wa Sheria wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali [Miscellaneous (Amendments) Bill 2014]; na
iv) Muswada wa Sheria Mpya ya
Kodi ya Ongezeko la Thamani [The Value Added Tax Act, 2014]
unaopendekeza kufuta Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani.
d) Maazimio
Mheshimiwa Spika,
10. Vilevile, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge pia walikubali Maazimio ya Bunge kama ifutavyo:
i) Azimio la kuridhia kubadilisha Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kuwa Taasisi inayojitegemea kiutendaji [Tengeru Institute of Community Development (Establishment Order, 2013)];
ii) Azimio la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Fedha na Uwekezaji (SADC Protocal on Finance and Investment);
iii) Azimio la Kuridhia Itifaki
ya Kuanzisha Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki [Protocol on
the Stablishment of the East African Community Monetary Union].
Kauli za Mawaziri
Mheshimiwa Spika,
11. Katika Mkutano huu pia Mawaziri waliweza kutoa Kauli za Serikali zifuatazo:
i) Kauli ya Waziri wa Maji Kuhusu Matatizo ya Uzalishaji Maji katika Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu;
ii) Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Kuhusu Ugonjwa wa Homa ya Dengue;
iii) Kauli ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Kuhusu Hali ya Mashine za Mionzi za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI).
SERIKALI ILIVYOJIPANGA KUTEKELEZA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI MWAKA 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
12. Wakati wa Mjadala wa Mpango na Bajeti ya Serikali ya
mwaka 2014/2015; Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili na kutoa
maoni na ushauri kuhusu Sera na Mikakati iliyopangwa na Serikali ya
kuimarisha maandalizi na usimamizi wa utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya
Serikali. Tunashukuru kwa michango hiyo mizuri ambayo Serikali inaahidi
kuifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika,
13. Napenda kutumia fursa hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge
wengine kuwapongeza Mheshimiwa Stephen Masato Wasira (Mb.) – Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu; na Mheshimiwa Saada Mkuya
Salum (Mb.) – Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha vizuri Hotuba za Mpango na
Bajeti ya Serikali na pia kutoa maelezo mazuri ya ufafanuzi wakati wa
kuhitimisha Hoja hii tarehe 24 Juni 2014. Vilevile, nawapongeza
Mawaziri wa Kisekta na Naibu Mawaziri kwa kuwasilisha Bajeti za Wizara
zao kwa umahiri mkubwa. Pamoja na pongezi hizo, napenda kutoa msisitizo
katika maeneo machache yafuatayo:
a) Kuimarisha utengemavu wa Viashiria vya Uchumi Jumla
Mheshimiwa Spika,
14. Ukuaji wa uchumi jumla ulio endelevu unahitaji mazingira
ya uchumi jumla yaliyotengamaa na yanayotabirika. Mwenendo wa ukuaji wa
uchumi katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ukiongezeka na kufikia
wastani wa Asilimia 7 kwa mwaka licha ya changamoto za upandaji bei za
chakula na mafuta ya petroli katika soko la dunia.
Ili kuweza kuendeleza
ukuaji huu mzuri wa uchumi hapana budi kuendelea kutengamaza vigezo
muhimu vya uchumi jumla, ikiwa ni pamoja na kuendeleza na kuimarisha
Ukuaji halisi wa Pato la Taifa na kukua kwa kiwango cha juu zaidi ya
Asilimia 7.0; kudhibiti kasi ya upandaji bei kwa kuhakikisha kwamba
kiwango cha mfumuko wa bei ni chini ya tarakimu moja, ikiwezekana
kisichozidi Asilimia 5; na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili
kupunguza utegemezi. Kutengamaza viashiria hivi kutaihakikishia Nchi
yetu kuendelea kwa kasi katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini hasa
ule wa kipato kwa Wananchi wetu wengi wa Vijijini.
Tayari dalili nzuri
zinaanza kujitokeza, kwani kiwango cha Watanzania walio katika umaskini
kimepungua kutoka Asilimia 33.6 mwaka 2007 hadi Asilimia 28.2 mwaka
2012. Aidha, wastani wa Pato la Mwananchi kwa mwaka limeongezeka kutoka
Shilingi 516,000 mwaka 2007 hadi Shilingi 1,003,000 mwaka 2012.
b) Kuimarisha utaratibu na usimamizi wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015
Mheshimiwa Spika,
15. Mwaka 2014/2015, ni wa Nne wa utekelezaji wa Mpango wetu
wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016). Ili kuhakikisha
kuwa utekelezaji wa Mpango unafikia malengo yaliyokusudiwa, Serikali
imeiagiza Tume ya Mipango kuendelea na utaratibu wa kukagua na
kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya Maendeleo ya
kipaumbele na ile ya kimkakati ili kuhakikisha kuwa inatekelezwa kwa
kuzingatia viwango vya ubora vilivyokubalika na inalingana na thamani ya
fedha zilizotolewa na Serikali (Value for money). Vilevile, kuhakikisha
kuwa Miradi hiyo inakamilika kwa wakati; na pale ambapo kuna changamoto
za kiutekelezaji kutoa ushauri stahiki Serikalini wa njia za
kufanikisha miradi husika. Kwa upande wa miradi inayotekelezwa katika
ngazi za Sekretariati za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ambayo
inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Serikali itaimarisha
mfumo wa ufuatiliaji kwa kuzingatia uzoefu uliopatikana katika mfumo wa
“Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” (Big Results Now – BRN).
Mheshimiwa Spika,
16. Sambamba na hatua hizo, napenda kulifahamisha Bunge lako
Tukufu kuwa, Serikali imeanza kufanya mapitio ya utekelezaji wa Mpango
wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016). Lengo la mapitio
hayo ni kupima hatua ya utekelezaji wa mpango na kubaini changamoto
pamoja na kuweka mikakati ya maandalizi ya Mpango wa Pili wa Maendeleo
wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021). Taarifa ya mapitio ya Nusu ya
Kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 –
2015/2016), itatolewa Desemba 2014. Madhumuni ya Taarifa hii ni
kuhakikisha kuwa maeneo ambayo hayakutekelezwa ipasavyo na maeneo mapya
yaliyoibuka (emerging issues) hususan kuiandaa nchi kwa uchumi wa gesi
na umuhimu wa kuimarisha ushindani wa Tanzania katika uzalishaji na
biashara ya Kimataifa.
c) Kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
17. Kutokana na michango mizuri ya mawazo ambayo Serikali
imepokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wakati wa Mjadala wa Bajeti ya
Serikali na Mafungu ya Wizara za Kisekta, Serikali imejipanga vizuri
zaidi kuimarisha ukusanyaji wa Mapato katika Mwaka 2014/2015. Hata
hivyo, ni vyema Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa kwenye eneo la mapato
yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Serikali ya awamu ya
nne imefanikiwa kuongeza mapato hayo kutoka Wastani wa Shilingi Bilioni
117 kwa mwezi Mwaka 2005/2006 hadi Wastani wa Shilingi Bilioni 800 kwa
Mwezi mwaka 2013/2014. Ongezeko hilo ni sawa na Asilimia 351. Lengo la
Serikali ni kuongeza kasi zaidi katika eneo hili hata kuzidi kiwango
hiki.
Mheshimiwa Spika,
18. Pamoja na kuipongeza TRA kwa jitihada hizo, Serikali
itafanyia kazi maoni mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge ya kupanua wigo
wa vyanzo vya Kodi pamoja na taarifa zilizopatikana zinazoonyesha kwamba
bidhaa nyingi zinapita kwenye bandari bubu au vituo vya forodha bila
kulipakodi stahiki. Hatua za kupunguza misamaha ya Kodi zitaendelea
kuimarishwa. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuielekeza Mamlaka ya
mapato Tanzania kuongeza ufanisi wa kiutendaji na kuimarisha zaidi
miundo ya ukusanyaji na ulipaji kodi. Ni muhimu, Mamlaka ya Mapato
kurahisisha zaidi taratibu za kukusanya Kodi kwa kuweka na kutangaza kwa
uwazi Kodi zinazostahili kulipwa kulingana na aina ya bidhaa na
kuondokana na utaratibu wa kufanya makadirio au kutumia mwanya wa
majadiliano na walipa kodi jambo ambalo linaweza kutoa mwanya kwa rushwa
na hivyo kuikosesha Serikali Mapato yake stahiki. Vilevile, naviagiza
Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutoa ushirikiano wa kutosha katika
kudhibiti na kuzuia ukwepaji wa kodi na ushuru katika bandari zetu na
maeneo ya mipakani.
Mheshimiwa Spika,
19. Ni imani yangu kuwa tukiweka wazi kodi zinazopaswa
kulipwa na tukirahisisha taratibu za kukusanya Mapato ya Kodi hususan
Bandarini na maeneo ya mipakani tutaweza kuweka mazingira mazuri ya
kusaidia kuongeza mapato ya Serikali na kupunguza urasimu na vishawishi
vya kudai Rushwa. Nashauri, Mamlaka ya Mapato Tanzania ijipange upya
vizuri ili kuhakikisha kwamba jukumu la kukusanya kodi linatekelezwa
vizuri na kwa weledi mkubwa. Tukiwa na uhakika wa makusanyo ya mapato
yetu ya ndani, naamini tutakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika,
21. Ili kuimarisha ukusanyaji wa Mapato yatokanayo na Kodi
na yasiyo ya Kodi (Non-Tax Revenue) na ya Halmashauri kuanzia Mwaka ujao
wa Fedha, Wizara zenye jukumu la kukusanya Kodi na Maduhuli pamoja na
makusanyo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala za Serikali, Idara za
Serikali zinazojitegemea kuanzia sasa zitatakiwa kuandaa Mpango Mkakati
na Mpango Kazi (Action Plan) wa mwaka wa kukusanya Mapato na Maduhuli
yao yote na kutoa taarifa bila kukosa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu kuhusu makusanyo ya kila robo mwaka; ifikapo tarehe 15 ya mwezi
unaofuata kila baada ya robo mwaka ambaye atawasilisha taarifa hiyo ya
utekelezaji kwenye Kamati Ndogo za Baraza la Kazi la Baraza la Mawaziri
zinazohusika kwa ajili ya tafakuri na maelekezo.
Mheshimiwa Spika,
22. Tayari Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu ameagizwa
kuandaa utaratibu mzuri wa kupata Taarifa za Makusanyo ya Mapato
yatokanayo na Kodi na Maduhuli kutoka Wizara na Taasisi zote za Serikali
zinazojitegemea. Aidha, naagiza kila Katibu Mkuu wa Wizara, Wakurugenzi
wa Halmashauri na Watendaji Wakuu wote wa Taasisi, Wakala za Serikali
na Idara za Serikali zinazojitegemea kuhakikisha zinakusanya Mapato
kulingana na Mpango Mkakati wa Mpango Kazi na kuwasilisha Taarifa hizo
kwa wakati.
MISAMAHA YA KODI
Mheshimiwa Spika,
23. Eneo la misamaha ya Kodi limekuwa likilalamikiwa na
Wananchi wengi na Waheshimiwa Wabunge kwa muda mrefu. Katika eneo hili,
ni vyema Wananchi na Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa kuna misamaha ya
Kodi ya aina mbalimbali. Kundi la Kwanza ni misamaha ya Kodi
inayotolewa kwa Washirika wetu wa maendeleo wanaotoa misaada katika
miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi linajumuisha pia misamaha ya
bidhaa za Sukari, Mchele, Mafuta ya Diseli, n.k. Kundi la Pili ni
misamaha ya Kodi kwa Asasi zisizo za Kiserikali na Mashirika ya Dini
yanayotoa huduma kwa Wananchi pasipo kutegemea kupata faida. Kundi la
Tatu ni misamaha ya Kodi ambayo hutolewa ikiwa ni Mkataba wa kuvutia
Uwekezaji Nchini. Kwa kawaida Misamaha ya aina hii hutolewa kupitia
Kituo cha Uwekezaji (TIC) ili kuvutia Uwekezaji katika Miradi Mikubwa
ambayo tunategemea kuwa manufaa yatakayopatikana kutokana na uwekezaji
huo yatakuwa makubwa sana ikilinganishwa na msamaha wa kodi uliotolewa.
Kwa mujibu wa Takwimu za hivi karibuni za Mamlaka ya Mapato Tanzania za
Mwaka 2012/2013 zinaonesha kuwa Misamaha ya Kodi ya bidhaa za mtaji kwa
Wawekezaji waliopewa Hati za Usajili na Cheti cha hadhi ya Uwekezaji
mahiri kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) ni Asilimia 19.7 ya Misamaha
yote.
24. Kwa mfano, utafiti
uliofanywa na Kituo cha Uwekezaji TIC mwaka 2012 kwa Makampuni Makubwa
50 ya Uwekezaji yaliyosajiliwa na TIC, kiasi kilichowekezwa katika
kipindi cha miaka mitano (2005 – 2010), ni Shilingi Trilioni 1.7 ambapo
katika uwekezaji huo, Makampuni hayo yalilipa Kodi Shilingi Trilioni
1.1. Aidha, Makampuni hayo yalitoa ajira 981,000 za moja kwa moja na
112,070 zisizo za moja kwa moja. Misamaha ya Kodi iliyotolewa kwa
Makampuni hayo ni Asilimia Saba (7) tu ya Kodi yote iliyolipwa na
Makampuni hayo. Misamaha kwa makundi mengine ikiwemo Miradi ya Wahisani
mbalimbali na Asasi zisizo za Serikali (NGOs), n.k ni Asilimia 38.6; na
Misamaha kwa Sekta Binafsi ni Asilimia 23.8 ya Misamaha yote
iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mheshimiwa Spika,
25. Serikali inatambua kuwa bado tuna kazi ya kubwa ya
kuhakikisha kwamba misamaha ya kodi inayotolewa kwa Wawekezaji na
Walengwa wengine Nchini inatumika vizuri katika miradi iliyokusudiwa, na
si vinginevyo. Kwa mfano, msamaha wa kodi uliotolewa kwenye mafuta ya
dieseli hatutarajii mafuta hayo yaingie sokoni badala ya kutumika kwenye
mradi wa uwekezaji uliokusudiwa. Hivyo, kutokana na umuhimu wa kuvutia
uwekezaji Nchini, misamaha ya kodi iiliyoidhinishwa na Bunge Kisheria
itaendelea kutolewa kwa Wahusika. Nitoe wito kwa wote watakaopata
misamaha hii kuwa waadilifu na kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yoyote atakayetumia vibaya
misamaha hii. Serikali kwa upande wake itaimarisha zaidi usimamizi wa
matumizi ya misamaha hii na itahakikisha inatumika kwa lengo
lililokusudiwa.
KUONDOA URASIMU KATIKA VITUO VYA FORODHA
Mheshimiwa Spika,
26. Mwezi Februari, 2014 nilipokutana na Wafanyabiashara
waliotaka kugoma kutumia Mashine za kisasa za kutoa Risiti (Electronic
Fiscal Devise-EFD) walinieleza kwamba moja ya eneo linalowasumbua ni
urasimu mkubwa katika maeneo mengi ya Vituo vya Forodha Mipakani na
Bandarini hasa Dar es Salaam. Katika Vituo hivyo vya Forodha walisema
zipo Taasisi nyingi za Serikali zinazofanya ukaguzi wa mizigo
inayoingizwa Nchini na ile inayotoka kwenda Nje ya Nchi. Miongoni mwa
Taasisi hizo ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); Idara ya
Uhamiaji; Jeshi la Polisi; Wakala wa Viwango (TBS); Mamlaka ya Udhibiti
wa Chakula na Dawa (TFDA); Mkemia Mkuu wa Serikali; Tume ya Nguvu za
Atomiki; Idara ya Misitu na Nyuki; Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Mimiea
na Wadudu (TPRI); Kitengo cha Afya ya Mimea cha Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika; na Kitengo cha Afya ya Mifugo cha Wizara ya
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Spika,
27. Serikali iliweka Taasisi nilizozitaja hapa kwa nia njema
ya kusimamia vizuri na kudhibiti uingizaji na utoaji wa mizigo
bandarini na bidhaa zinazopitishwa katika mipaka ya Nchi yetu. Hata
hivyo, baadhi ya Watendaji wasio waaminifu wanatumia mwanya huo
kuwalazimisha Wafanyabiashara kutoa fedha zao bila kupata risiti eti kwa
ajili ya kusaidia mizigo kupitishwa kwa urahisi. Aidha, nimeelezwa kuwa
baadhi ya Watendaji wanatumia nafasi zao kuongeza urasimu usio na
lazima ili kudai rushwa, jambo ambalo linaongeza gharama kwa
Wafanyabiashara na kuleta athari za kuchelewesha utoaji wa mizigo
bandarini na kuathiri sifa za bandari zetu.
Naagiza Wizara husika
kufuatilia utendaji kazi wa Vyombo hivyo kwa karibu na kushughulikia kwa
haraka malalamiko mbalimbali na kupata ufumbuzi wa tatizo la urasimu
katika Vituo vya Forodha. Yapo Makampuni ya Mawakala yapatayo 527
yanayofanya kazi za Mawakala wa kutoa bidhaa Bandarini. Tunayo taarifa
kuwa, Utitiri wa Makapuni hayo nao umekuwa chanzo kikubwa cha rushwa na
ukwepaji Kodi. Serikali haikubaliani na aina hii ya Utendaji wa
Makampuni hayo. Utendaji huo uachwe sasa. Navitaka Vyombo husika
kufuatilia kwa karibu sana mienendo ya Makampuni yote ya Mawakala wa
kutoa bidhaa Bandarini na kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Spika,
28. Pamoja na changamoto zilizopo katika bandari zetu,
napenda kutumia fursa hii kumpongeza Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt.
Harrison Mwakyembe (Mb.) kwa kazi kubwa anayofanya ya kusimamia kwa
karibu uboreshaji wa utendaji katika Mamlaka ya Bandari; hasa kupunguza
muda wa kutoa mizigo bandarini kutokana na kuweka utaratibu wa kufanya
kazi kwa saa 24. Ninamtaka aongeze juhudi zaidi ili kuimarisha utendaji
kazi katika eneo hili ili kuongeza sifa kwa Bandari zetu.
UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG RESULTS NOW-BRN)
Mheshimiwa Spika,
29. Utekelezaji wa mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa umeendelea vizuri, na licha ya matatizo ya upatikanaji wa fedha matokeo yake yameanza kuonekana kama ilivyoainishwa na Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta husika walipowasilisha Hotuba zao katika Mkutano huu. Uzoefu tulioupata katika kipindi hiki, ni kwamba upatikanaji wa matokeo makubwa kwa muda mfupi unawezekana, ilimradi tuwe tumechagua vipaumbele vyetu kwa usahihi, tunafuatilia utekelezaji kwa karibu, na kutanzua changamoto mara zinapojitokeza. Napenda kutumia fursa hii tena kuwashukuru Wadau wote wa Maendeleo waliowezesha kupata matokeo haya. Natoa wito kwa Viongozi na Watendaji katika ngazi zote tuendeleze kasi na umakini wa kufuatilia utekelezaji wa Miradi ya kipaumbele ya Mfumo wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” ili tuweze kufanikiwa zaidi katika kipindi kijacho.
Mheshimiwa Spika,
30. Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba katika
Mwaka 2014/2015, Serikali itakamilisha mchakato wa Ajira za nafasi wazi
za Watumishi wa Taasisi ya Kuratibu na Kusimamia Mfumo wa Tekeleza sasa
kwa Matokeo Makubwa kilichopo Ofisi ya Rais, yaani President’s Delivery
Bureu (PDB). Vilevile, Serikali itaimarisha Vitengo na Taasisi zote
zinazosimamia mfumo huu, ikiwa ni pamoja na kukamilisha uundaji wa
Vitengo na Kamati za kuratibu utekelezaji katika Wizara na Taasisi
zinazotekeleza Programu ya Uboreshaji wa Mazingira ya Biashara Nchini.
Serikali pia itaandaa na kutangaza matokeo ya utekelezaji wa mfumo huu
katika mwaka wake wa kwanza wa 2013/2014, baada ya kuhakikiwa na jopo
huru la Kimataifa. Hatua hii inalenga kukamilisha mfumo wa uwajibikaji
ambao ni chachu muhimu ya mafanikio ya mfumo wa Tekeleza Sasa kwa
Matokeo Makubwa. Vilevile, Wizara zingine, Mikoa na Halmashauri zote
zinaendelea kuhimizwa kutumia mfumo huu katika kuchambua, kupanga, na
kutekeleza mipango na miradi yake yote ya maendeleo kwa kuzingatia mfumo
huu wa Matokeo Makubwa Sasa.
KILIMO
Hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini
Mheshimiwa Spika,
31. Hali ya upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuwa ya
kuridhisha katika maeneo mengi kufuatia albaki ya mavuno ya msimu
uliopita na matarajio ya mavuno mazuri katika msimu wa kilimo wa
2013/2014 ambayo uvunaji wake umeanza katika baadhi ya maeneo. Aidha,
kufuatia mwenendo mzuri wa hali ya unyeshaji wa mvua katika msimu wa
2013/2014 katika maeneo mengi ya nchi, kuna matarajio ya uzalishaji
mkubwa wa mazao ya chakula na hivyo upatikanaji mzuri zaidi wa chakula
kwa mwaka 2014/2015.
Mheshimiwa Spika,
32. Hali ya akiba ya chakula katika Maghala ya Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula ni nzuri. Mwanzoni mwa mwaka 2013/2014 Akiba
ya Chakula ilikuwa Tani 25,452.6 na baada ya kununua Tani 219,377.3,
akiba ilifikia Tani 244,829.9. Hadi kufikia tarehe 4 Juni 2014 Serikali
ilitoa Jumla ya Tani 54,845.0 kama chakula cha Msaada na Maafa ikiwemo
njaa, mafuriko na operesheni mbalimbali na kubaki na akiba ya Tani
189,984.9. Aidha, Serikali ina mpango wa kuuza Tani 75,000 ili kuacha
Maghala wazi kwa ajili ya mazao mapya yatakayonunuliwa katika msimu mpya
wa 2014/2015 na hivyo, kuyaacha Maghala ya Serikali yakiwa na Akiba ya
Tani 114,984.9 za Mahindi ifikapo Julai, 2014. Katika mwaka 2014/2015
Serikali itanunua Tani 160,000 za Nafaka na kuzijumlisha zile za akiba
kutoka msimu wa 2013/2014, hivyo kuwa na hifadhi ya jumla ya Tani
274,984.9 za Nafaka.
Mheshimiwa Spika,
33. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu na Wananchi kuwa
Serikali kwa mara ya kwanza imefikia uamuzi wa kununua Mpunga na
kuhifadhi katika Maghala ya Taifa kama Chakula cha Akiba. Uamuzi huu
umefikiwa kwa kuzingatia kuwa baada ya Serikali kuruhusu wafanyabiashara
kuingiza mchele kutoka nje ya Nchi kufidia pengo la upungufu wa mchele
hapa Nchini, baadhi ya wafanyabiashara hao waliendelea kuingiza mchele
hata baada ya muda wa vibali vyao kuisha hivyo kuwafanya Wakulima kukosa
soko la mpunga baada mavuno kuongezeka. Napenda kulijulisha Bunge lako
Tukufu kuwa katika msimu huu wa mavuno, Serikali imedhamiria kuanza na
hifadhi ya Tani 10,000 za mpunga kwa lengo la kujiridhisha kama hifadhi
ya mpunga haitakuwa na matatizo. Baada ya kujiridhisha, katika misimu
inayofuata, Serikali itaongeza kiasi cha Mpunga utakaohifadhiwa na
Serikali kwa nia ya kuziba pengo la upungufu wa mchele iwapo hali hiyo
itatokea badala ya kutegemea Wafanyabiashara tu kuagiza Mchele kutoka
nje ya Nchi. Nitumie fursa hii kuwahimiza wakulima kuongeza uzalishaji
wa zao hili kwa vile sasa Serikali imeamua kuhifadhi Mpunga kama ilivyo
kwa Mahindi na Mtama. Aidha, niwaahidi Wananchi kuwa Serikali itaendelea
kuboresha miundombinu ya kuhifadhi mpunga katika Maghala ya Taifa ili
kuwawezesha Wakulima wengi kupata soko kama ilivyo kwa mazao ya Mahindi
na Mtama. Ninaagiza kuanzia sasa Taasisi zote zinazotoa vibali vya
kuingiza sukari, mchele na ngano kutoka nje ya nchi kuhakikisha kuwa
Wafanyabiashara wenye vibali vinatumika tu kwa muda uliopangwa.
Mheshimiwa Spika,
34. Naagiza pia kwa Wakala wa Hifadhi Taifa ya Chakula kuanza
kununua nafaka kwa wakati ili wakulima waweze kunufaika na bei nzuri
zitakazotolewa. Ni matarajio yangu kuwa Wakala pamoja na kununua nafaka
kwa bei ya soko na kupitia vituo vya ununuzi, vikundi vya wakulima na
mawakala, watahakikisha kuwa wakulima hasa wa mahindi wanapata si chini
ya Shilingi 500 kwa kilo ambayo ni bei ya msimu uliopita ili
kuwawezesha kurudisha gharama za uzalishaji. Aidha, nawasihi Wakulima
wasikubali kuuza mazao yao chini ya bei hiyo. Lengo ni kuwawezesha
kurejesha gharama za uzalishaji. Bei elekezi kwa nafaka nyingine pia
zitangazwe kwa kuzingatia gharama za uzalishaji mapema kabla ya msimu wa
ununuzi kuanza. Nichukue fursa hii kuwasihi Wananchi hasa katika Kanda
zile wanazouza nafaka iliyo na ubora hafifu hasa uchafu kujirekebisha na
kuacha tabia hiyo mara moja, kwani kwa kufanya hivyo wanavuruga
jitihada za Serikali za kusaidia Wakulima Wadogo kuinua maisha yao.
Mazao ya Asili ya kuingiza Fedha za Kigeni
Mheshimiwa Spika,
35. Nchi yetu inayo mazao yanayotuingizia fedha za kigeni
ikiwa ni pamoja na Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Tumbaku n.k. Kwa
madhumuni ya Hotuba yangu ya leo nimeona nizungumzie uendelezaji wa
mazao ya Korosho na Pamba. Kutokana na bei ya mazao haya kuendeea
kutegemea bei katika Soko la Dunia, Wakulima wetu wameendelea kupata bei
za chini na zisizokuwa na uhakika kila msimu wa mauzo unapowadia.
Hivyo, ni vyema sasa tukazingatia umuhimu wa kuweka mikakati ya
kuhakikisha kuwa soko la ndani linakuwa la uhakika kwa mazao haya.
Aidha, Serikali imekuwa ikiweka mikakati ya kusindika mazao ya Pamba na
Korosho hapa Nchini kwa lengo la kuyaongezea thamani na kuongeza Tija
katika uzalishaji kwa eneo. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali sasa
imejikita katika utafiti wa mbegu na miche bora pamoja na kufufua
viwanda ambavyo vitatumia malighafi zitokanazo na mazao haya hapa
Nchini.
Mapango wa kufufua Viwanda vya Korosho
Mheshimiwa Spika,
36. Uzalishaji wa korosho umeendelea kuwa tegemeo kubwa la
wakulima wa Mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara na pia Mkoa wa Pwani.
Kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali za kufufua zao hili, katika
msimu wa 2013/2014, uzalishaji wa Korosho umeongezeka hadi kufikia Tani
127,939.4 ikilinganishwa na Tani 121,703.8 kwa msimu wa 2012/2013.
Pamoja na ongezeko katika uzalishaji, mchango wa zao hili kwa Pato la
Mkulima na Taifa umekuwa mdogo kutokana na Taifa kuendelea kuuza korosho
ghafi nje ya Nchi kwa zaidi ya Asilimia 90 hivyo, kuikosesha Nchi
mapato na faida nyingine nyingi kwa wakulima. Hali hii imetokana na
Wawekezaji wa Viwanda 12 vya kubangua korosho vilivyojengwa na Serikali
miaka ya 1980 na kubinafsishwa mwaka 2004 kushindwa kuvifufua viwanda
hivyo kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa mitaji na
kuendelea kutumia Teknolojia iliyopitwa na wakati.
Mheshimiwa Spika,
37. Napenda kulijulisha Bunge lako na wananchi kwamba
kutokana na changamoto hizo, mwezi Februari, 2014 niliitisha Kikao
kilichohusisha baadhi ya Watendaji Wakuu wa Serikali, baadhi ya Wamiliki
wa Viwanda vya kubangua Korosho na baadhi ya Taasisi ya Fedha kujadili
mikakati ya kufufua viwanda vya kubangua korosho hapa nchini. Hivyo,
Serikali kwa kushirikiana na wadau hao iliamua ifanyike tathmini ya
gharama na mikakati ya kufufua Viwanda vya kubangua korosho hatua kwa
hatua na kwa kuanzia Serikali kwa kushirikiana na Wamiliki itaanza
kufufua Viwanda vinne (4) vyenye uwezo wa uzalishaji (Installed
Capacity) wa kati ya Tani 5,000 hadi 10,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika,
38. Kwa kuanzia Serikali iliamua tathmini ifanyike kwa
viwanda vya Newala-I; Masasi; Lindi Farmers kilichopo Nachingwea; na
Kiwanda cha Kampuni ya BUCCO kilichopo Lindi kwa ushirikiano kati ya
Serikali na Kampuni ya Oltremare ya Italy ambayo ina uzoefu mkubwa
duniani katika utengenezaji wa mashine za usindikaji wa Korosho. Kampuni
hii ndiyo iliyojenga baadhi ya viwanda vya kubangua korosho hapa nchini
kikiwepo Kiwanda cha TANITA. Tathmini hii itaangalia hali ilivyo katika
masuala ya kiufundi, usindikaji na miundombinu; uwezo na madeni ya
Kifedha; Masuala ya Kisheria kuhusu Mikataba mbalimbali iliyowekwa na
wawekezaji hawa, Mfumo wa upatikanaji wa malighafi; na uwezo wa
Rasilimali watu wa viwanda hivyo.
Mheshimiwa Spika,
39. Tathmini ya awali ya gharama za kufufua viwanda hivyo
vinne iliyofanywa na Kampuni ya Oltremare kwa kushirikiana na Kampuni ya
Agrofocus ya hapa Tanzania ilibaini kuwa kuna njia mbili zinazoweza
kutumika: Kwanza, iwapo Serikali itaamua kuvifufua Viwanda vya Newala 1;
Masasi na Lindi kwa kuvijengea uwezo wa kila kimoja kubangua Tani
15,000 kwa mwaka, pamoja na cha Nachingwea kubangua Tani 7,500 kwa
mwaka; kwa pamoja zitahitajika jumla ya Paundi 31,280,690. Pili, iwapo
Serikali itaamua kuvifufua viwanda vya Newala 1, Masasi na Lindi kwa
kuvijengea uwezo wa kila kimoja kubangua Tani 22,000 kwa mwaka, na
Kiwanda cha Nachingwea kubangua Tani 7,500 kwa mwaka, kwa pamoja
zitahitajika jumla ya Paundi 44,185,022. Hata hivyo, kabla ya kuweka
mikakati ya kupata fedha hizo, Serikali imeamua kupeleka kikosi kazi
chake kutathmini tena gharama hizo na kuzilinganisha na hizo za awali
kwa nia ya kushirikiana na vyombo vya fedha na Kampuni ya Oltremare ya
Italy kufufua viwanda hivi. Aidha, Kampuni ya Oltremare ya Italy
imekubali kutoa mafunzo kwa wazawa kuhusu utawala na uendeshaji wa
viwanda hivyo pindi vitakapofufuliwa; na kuisaidia Tanzania kupata Soko
la Korosho zitakazobanguliwa. Naamini kabisa ufufuaji wa viwanda hivi
utasaidia kuboresha teknolojia, kuongeza ufanisi, ajira na mapato ya
Serikali na bei ya korosho ghafi kwa mkulima badala ya kutegemea bei ya
Soko la Dunia pekee.
Zao la Pamba
Mheshimiwa Spika,
40. Zao la Pamba lina mchango mkubwa katika kukuza Uchumi wa
Nchi yetu na kuondoa umaskini kwa zaidi ya Wakulima 400,000 na
wategemezi wao katika Mikoa takriban 15 hapa Nchini. Hata hivyo, bado
Kilimo chake kinakabiliwa na changamoto nyingi. Baadhi ya changamoto
hizo ni pamoja na tija ndogo, matumizi kidogo ya teknolojia za kisasa na
zana duni. Aidha, kuna huduma duni za ugani na utafiti, kukosa mitaji
na soko la uhakika; migogoro baina ya wakulima na wafanyabiashara, na
Uhaba wa Viwanda vya kuongezea Pamba thamani.
Mheshimiwa Spika,
41. Katika msimu wa 2011/2012 Serikali kwa kushirikiana na
Shirika la Gatsby Charitable Foundation ya Uingereza chini ya Ufadhili
wa Lord David Sainsbury ilianza majaribio ya Mfumo wa Kilimo cha Pamba
cha Mkataba kupitia Program ya Kuendeleza zao la Pamba katika Mkoa wa
Mara na Wilaya za Bariadi na Kibondo kwa madhumuni ya kutafuta ufumbuzi
wa changamoto nilizoeleza punde. Matokeo ya majaribio yalionesha kuwa,
uzalishaji uliongezeka kutoka Kilo 398 kwa ekari hadi Kilo 558 kwa
ekari; na ubora wa pamba uliongezeka hadi kufikia Asilimia 78 kutoka
Asilimia 48 za awali.
Mheshimiwa Spika,
42. Baada ya Serikali kupitia Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuanza
mikakati ya kusimamia kilimo cha Mkataba cha pamba, takwimu za mwezi
Mei, 2014 zinaonesha kuwa Wilaya Saba (7) katika Kanda ya Magharibi
zilishiriki katika Kilimo cha Mkataba. Aidha, takriban wakulima 90,000
wamenufaika na mikopo ya Pembejeo ya Kilimo cha Mkataba msimu huu
kupitia Wachambuzi takriban 15, ikilinganishwa na wakulima 30,000 katika
msimu uliopita. Vilevile, takwimu hizo zinaonyesha wakulima 140,000
ndani ya kilimo cha mkataba wamelima zaidi ya ekari 400,000; na kwamba
katika msimu huu kati ya Makampuni 42 ya pamba, Makampuni 26,
yameshiriki kwenye kilimo cha mkataba ikilinganishwa na Makampuni 12
yaliyoshiriki msimu uliopita. Kwa ujumla wakulima wengi wameelezea
kunufaika kutokana na Kilimo cha Pamba cha Mkataba hasa kutokana na
kuongezeka kwa kipato.
Mheshimiwa Spika,
43. Pamoja na mafanikio hayo, yaliyojitokeza changamoto
kadhaa ikiwepo ya baadhi ya Wakulima kuuza na Makampuni kununua pamba
nje ya mkataba jambo lililokwamisha Mfumo wa kurudisha mikopo ya
pembejeo katika maeneo yaliyolimwa kwa mfumo wa Kilimo cha Mkataba.
Hivyo, Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya
kusimamia utekelezaji wa Kilimo cha Mkataba kwenye zao la pamba katika
maeneo yote yanayolimwa pamba. Lengo ni kushirikisha Wadau wengine,
kuainisha na kupata ufumbuzi wa kasoro zilizojitokeza katika misimu
iliyopita; kupanga mikakati ya utekelezaji; kuweka utaratibu mzuri wa
kulinda uwekezaji wa wachambuaji na pia kulinda haki za wakulima kwa
kuzingatia mikataba inayowekwa kati ya wakulima na wachambuaji. Nitumie
fursa hii kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutekeleza agizo la
Mheshimiwa Rais kwa Viongozi kusimamia kikamilifu kazi hiyo ili Wakulima
wanufaike na Mfumo huu wa Kilimo cha Mkataba. Njia nyepesi ya kutoa
elimu juu ya Kilimo cha Mkataba ni kutumia Mashamba Darasa na Mashamba
ya Mfano. Nawaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi Watendaji wa
Halmashauri wasimamie vema na kwa karibu utaratibu huu.
Mheshimiwa Spika,
44. Kutokana na tatizo lililojitokeza la baadhi ya wakulima
wa pamba kuuziwa Tani 1,088 za mbegu ya pamba kipara ambayo haikuota
kutoka Kampuni ya Quton, kwa niaba ya Serikali napenda kuwapa pole
Wakulima hao. Kama Serikali ilivyoahidi hapo awali, tumesitisha malipo
ya Shilingi Bilioni 1.7 za ruzuku kwa Kampuni ya Quton. Aidha, Serikali
inaitaka Kampuni ya Quton kutorudia makosa haya katika siku zijazo.
Maafisa Ugani wasimamie kwa karibu upandaji wa mbegu hizi wakati wa
msimu kwa kutoa elimu stahiki.
Mheshimiwa Spika,
45. Katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili la
mbegu hafifu, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara
ya Kilimo, Chakula na Ushirika inaendelea na juhudi za kukaribisha
uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha mbegu bora kipara kutoka ndani na
nje ya Nchi ili kuweka mazingira ya ushindani ambao utaleta ubora
zaidi. Aidha, Taasisi zinazohudumia zao la pamba ziangalie kama kuna
uwezekano wa kupata mbegu za pamba hata kutoka nje ya Nchi kwa
kuzingatia masuala ya ubora na unafuu wa bei. Nichukue fursa hii
kuwakumbusha Bodi ya Pamba na wagani wa zao la pamba kuhakikisha kuwa
ubora wa mbegu (germination percentage) unafanyiwa tathmini kabla mbegu
hazijagawiwa kwa wakulima. Aidha, Wakulima waelimishwe manufaa ya
kutumia Mbegu Kipara kwamba wakati wa kuziandaa zinawekewa viuatilifu
ambavyo vinaua vimelea na wadudu ambao wanatokana na mavuno ya msimu
uliopita, hivyo kupunguza uwezekano wa pamba inayotokana na mbegu hizi
kupata magonjwa na wadudu mapema ikilinganishwa na mbegu za manyoya.
46. Mbegu Kipara zinaweza pia
kutumika na mashine za kupandia (planter) hivyo kuwezesha mimea ya pamba
kuota katika mstari na kwa nafasi stahili na kumwezesha mkulima kupata
mimea mingi kwa ekari (plant population) kama inavyoshauriwa kitaalamu
miche 22,222, hivyo kuongeza tija kwa ekari tofauti na mbegu za manyoya.
Naamini kupitia ushirika na Kilimo cha Mkataba Wakulima wataweza
kuungana kupata planter ili kupunguza sulubu ya jembe la mkono wakati wa
kupanda. Ninaiagiza Bodi ya Pamba iendelee kusimamia zoezi la wakulima
waliochaguliwa kuzalisha mbegu bora kwa Kampuni ya Quton ili kuwezesha
ongezeko la upatikanaji wa mbegu bora kwa Wakulima.
Mheshimiwa Spika,
47. Pamoja na changamoto zinazoikumba tasnia ya pamba na hasa
Kilimo cha mkataba cha pamba, nichukue fursa hii kuwasihi wakulima wa
pamba ambao hawajajiunga na mfumo huu kufanya hivyo kutokana na
mafanikio yaliyopatikana kwa wale waliojiunga tayari. Napenda
kuwakumbusha Wagani wa Pamba kusimamia ipasavyo suala la usafi wa
pamba inayouzwa na wakulima ili wakulima wapate bei nzuri. Aidha,
kutokana na kilimo cha mkataba katika zao la tumbaku na mfumo wa
stakabadhi ya mazao ghalani kwa zao la korosho kuwanufaisha sana
wakulima wa mazao hayo, niwatake viongozi wote wanaohusika na
uimarishaji wa zao la pamba kuimarisha kilimo cha pamba na suala la
kilimo cha pamba cha mkataba ili kuweka utaratibu utakaomfanya mkulima
kuuza pamba kwa yule aliyemwezesha kupata pembejeo na kwa kutumia mfumo
wa Ushirika.
Mheshimiwa Spika,
48. Kupitia Mkutano Mkuu wa Wadau wa Sekta ya Pamba wa tarehe
4 Julai 2013 Jijini Mwanza, wajumbe waliiomba Serikali kusimamia
uanzishwaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya zao la pamba na
utengenezaji wa bidhaa za pamba hapa Nchini. Nakubaliana na azimio hilo
kwa sababu hatuwezi kama nilivyoeleza kwa zao la Korosho, kuendelea
kusafirisha sehemu kubwa ya pamba inayozalishwa hapa nchini kama
malighafi kwa vile hakutainufaisha nchi na hata wakulima. Hivyo, narudia
tena wito wangu kuitaka Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kuhimiza
uwekezaji katika viwanda vingi vya kusindika na kutengeneza bidhaa za
pamba hapa Nchini badala ya kuuza pamba ghafi. Napenda kulijulisha Bunge
lako Tukufu na Wananchi kuwa, katika kujiandaa na Raslimali Watu kwa
ajili ya Viwanda vya Nguo hapa Nchini, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam
kimewezeshwa kuanzisha Kozi za Shahada mbili za Uhandisi wa Viwanda vya
Nguo na Ubunifu, na Vyuo vya VETA vinatoa mafunzo hayo kwa Kada za
Chini.
Mheshimiwa Spika,
49. Kwa kuwa msimu wa ununuzi wa Pamba mwaka 2014/2015
umeshazinduliwa tangu tarehe 18 Juni, 2014, ninawasihi Wakuu wa Mikoa
yote inayolima pamba kusimamia kwa karibu mambo yafuatavyo:
Kwanza: Kuhakikisha kuwa bei ya chini ya kununua Pamba inakuwa Shilingi 750 kwa kilo;
Pili: Kuhakikisha kuwa maeneo
yote ambayo Bodi ya Pamba itathibitisha kwamba hakuna mnunuzi aliyetoa
huduma au mkopo kwa Mkulima, yawe huru kwa mnunuzi yeyote kupewa Leseni
ya kununua Pamba ili kuwapa fursa Wakulima ambao hawapo katika mfumo wa
kilimo cha mkataba kuuza bila matatizo.
50. Ni matumaini yangu kwamba, hatua hizi zitasaidia kwa kiasi kikubwa uboreshaji wa zao la Pamba.
UMUHIMU WA VIWANDA NA KULINDA VIWANDA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
51. Maendelea ya Nchi yoyote ile yanategemea sana ujenzi wa
viwanda. Kwa maana hiyo, suala la ujenzi wa viwanda haliepukiki
kutokana na sababu kwamba, Viwanda husaidia kuongeza thamani mazao ya
Kilimo, Mifugo, Uvuvi na mazao ghafi yanayozalishwa katika Sekta
zingine. Aidha, Viwanda huongeza muda wa bidhaa hizo wa kutumika kabla
ya kuharibika. Vilevile, mazao yaliyoongezwa thamani humpatia mkulima
bei nzuri na kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa mazao. Uwepo wa
viwanda pia unatusaidia kupata fedha za kigeni, kutoa ajira na hivyo
kupunguza tatizo la ajira kwa watu wetu hasa Vijana. Kwa maana hiyo kuna
haja ya kuwepo Sera na Sheria mahsusi zitakazohimiza na kuchagiza
uwekezaji katika Sekta ya Viwanda na pia kuondoa vikwazo vya kibiashara.
Mheshimiwa Spika,
52. Kwa kutambua umuhimu wa viwanda Nchini, ndio maana
Serikali imeanzisha Mpango wa uanzishaji wa Maeneo Maalum ya Uzalishaji
kwa Mauzo Nje Export Processing Zones – (EPZ) na Maeneo Maalum ya
Kiuchumi Special Economic Zones – (SEZ) kama mkakati mahususi wa
kuvutia Wawekezaji. Katika kipindi cha mwaka 2012 na 2013 jumla ya
miradi ya viwanda ipatayo 52 yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni
474.37 ilisajiliwa na Mamlaka ya EPZ ambapo ajira 12,347 za moja kwa
moja zinatarajiwa kupatikana. Aidha, katika kipindi cha Januari hadi Mei
2014, pekee jumla ya miradi 21 yenye thamani ya Dola la Kimarekani
Milioni 121.4 inayotarajia kutoa ajira za moja kwa moja zipatazo 4,814
imesajiliwa. Katika miradi hiyo, ipo Miradi inayosajiliwa kwa utaratibu
wa kushirikisha Sekta ya Umma na Binafsi (Private Public
Partnership-PPP). Ujenzi wa miradi hiyo iko katika hatua mbalimbali za
utekelezaji.
Mheshimiwa Spika,
53. Ni kweli kwamba, Serikali imeweka juhudi kubwa katika
ujenzi wa Viwanda katika sehemu mbalimbali Nchini na pia kupanua wigo wa
bidhaa zinazozalishwa. Kwa mfano, hivi sasa kuna Viwanda vya Chuma
takriban 17 vinavyojumuisha Viwanda vya mabati, misumari, nyaya za uzio,
nyaya za umeme, bidhaa za chuma, ikiwemo nondo na mabomba ya chuma kwa
ajili ya matumizi mbalimbali. Lakini pia tunavyo Viwanda vya kuzalisha
Saruji vipatavyo vitano (5) vya Dar es Salaam, (TPCC), Tanga (TCC),
Mbeya (MCC), Pwani (Rhino Cement Mkuranga), na Lindi (Lee Building
Material ya Kilwa Masoko). Vilevile, Viwanda Vipya vya Saruji vinajengwa
Arusha, Dar-es-Salaam (3), Tanga (2), Lindi, Pwani na Mtwara. Upanuzi
huu wa Viwanda vya Saruji vitaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa Nchi
Wazalishaji Wakuu Barani Afrika na hivyo kujitosheleza Kitaifa na kuuza
nje.
54. Tunavyo pia Viwanda vikubwa
vya Kusindika Ngozi Saba (7) katika Mikoa ya Arusha, Dar-es-Salaam,
Kilimanjaro (2), Morogoro, Pwani na Shinyanga. Tunavyo Viwanda vya Nguo
Tisa (9) katika Mikoa ya Arusha, Dar-es-Salaam (4), Mara, Morogoro,
Mwanza na Tanga na tunavyo pia Viwanda vya Sukari katika Mikoa ya
Kilimanjaro, Kagera na Morogoro ambavyo vyote kwa ujumla wao vina
mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Spika,
55. Pamoja na jitihada kubwa iliyowekezwa katika ujenzi wa
Viwanda hivyo Nchini, tunayo Changamoto kubwa ya namna ya kuvilinda
Viwanda hivi dhidi ya ushindani usio halali (Unfair Competition) ili
viweze kukua na kuimarika kiushindani, Kikanda na Kimataifa. Mathalani,
zipo bidhaa au vifaa vinavyoingizwa Nchini na kuuzwa kwa bei ya chini
ikilinganishwa na bei ya bidhaa aina hiyo hiyo zinazozalishwa Nchini.
Bidhaa hizo huuzwa kwa bei ya chini kutokana na wazalishaji wa Nchi
zinakotoka bidhaa husika kupewa ruzuku au bidhaa hizo zinakuwa na ubora
duni usiokidhi Viwango vya Ubora au kutozwa ushuru mdogo au kupewa
msamaha wa ushuru. Hali hii husababisha ushindani usio wa haki katika
Soko la Ndani na ni changamoto kubwa kwa Taifa letu na Afrika Mashariki
kwa ujumla. Naomba uniruhusu nitoe mifano michache ambayo itatuwezesha
kuona ni namna gani tunaweza kukabili changamoto hii kwa lengo la
kulinda Viwanda vyetu Nchini.
Mheshimiwa Spika,
56. Nikianza na Saruji. Kama nilivyosema tunavyo Viwanda
vitano vya Saruji vyenye uwezo wa kuzalisha Saruji hadi Tani Milioni 3.8
kwa mwaka. Mahitaji ya Saruji kwa sasa ni Tani Milioni 3.9 kwa mwaka na
zipo juhudi za kuongeza uzalishaji kupitia uwekezaji katika miradi tisa
(9) mipya ya ujenzi wa Viwanda vya Saruji ambavyo kwa ujumla wake
inatarajiwa vitazalisha Tani Milioni 8.3 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika,
57. Pamoja na uzalishaji huo mkubwa, changamoto kubwa ni
namna ya kuhimili gharama kubwa za uzalishaji wa Saruji ikiwemo umeme,
gharama za usafirishaji, na ushindani mkubwa dhidi ya saruji kutoka nje
ya nchi ambayo ina ruzuku, hivyo kuvuruga soko la ndani kwa Viwanda vya
Saruji. Aidha, ziko taarifa za ukwepaji kodi na udanganyifu ambao
umeendelea kuwa tatizo kubwa sana katika Sekta ya Saruji. Kwa kutambua
changamoto hiyo, Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilikubaliana
kuweka Ushuru wa Forodha wa Asilimia 55 mwaka 2005 na kuushusha kufikia
Asilimia 35 mwaka 2010. Matarajio yalikuwa ni kuvilinda Viwanda hivi ili
vijijenge kwa miaka mitano na baada ya hapo kuendelea kuvilinda kwa
kuviweka chini ya kundi la bidhaa nyeti, yaani kuwa na wigo wa pamoja wa
Ushuru wa Forodha wa zaidi ya Asilimia 25.
Mheshimiwa Spika,
58. Hali iliyojitokeza katika Viwanda vya Saruji
haitofautiani sana na Viwanda vya Chuma ambavyo navyo vina changamoto
kubwa hasa katika uzalishaji na ubora wa bidhaa za chuma. Mathalan, ziko
taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba karibu Viwanda vyote vya Nondo
Nchini vinazalisha chini ya viwango, jambo ambalo halikubaliki kabisa.
Nilibahatika kufanya Ziara Mkoa wa Mwanza ambapo nilikuta katika Mradi
mmoja wa ujenzi wa Tanki la Maji – Mkandarasi alikuwa ananunua Nondo
kutoka Uganda kwa madai kuwa Nondo zilizokuwa zinazalishwa na Viwanda
vyetu kwa maelezo yake zilikuwa chini ya viwango.
Kiwango stahiki
kinapaswa kuwa BS 406, BS 500, n.k. lakini Viwanda vyetu vinazalisha
chini ya kiwango hicho, yaani BS 400. Ni wakati muafaka sasa Viwanda
vyote kuzingatia viwango vya Kimataifa ili kuepusha majanga yanayotokana
na udhaifu huo na pia kuwezesha Nondo hizo kutumiwa na wahitaji wote wa
hapa ndani na nje ya Nchi. Ninahimiza Shirika la Viwango Nchini
liendelee kusimamia ubora wa bidhaa za Nondo kwa maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
59. Kwa sasa kuna Viwanda vya Nondo takriban 15 ambavyo vina
uwezo wa kuzalisha Nondo Tani 420,000 kwa mwaka. Mahitaji ya Nondo ni
Tani 200,000 kwa mwaka, ikiwa ni ziada ya Asilimia 40 zaidi ya mahitaji.
Aidha, Viwanda hivi vya Nondo peke yake vinatoa ajira ya moja kwa moja
ya watu 4,000 na wengine takriban 40,000 ambao siyo wa moja kwa moja.
60. Lakini pia tuna Viwanda
vikubwa vya Chuma viwili (2) vyenye uwezo wa kuzalisha Mabati Tani
150,000 kwa mwaka, wakati mahitaji ni Tani 100,000 kwa mwaka ikiwa ni
ziada ya Tani 50,000, sawa na Asilimia 50 ya mahitaji. Viwanda hivi
navyo vimezalisha ajira ya takriban Watu 16,000.
Mheshimiwa Spika,
61. Mifano hiyo miwili ya Uzalishaji wa Nondo na Mabati
inadhihirisha kwamba tatizo la uzalishaji kukidhi mahitaji halipo, bali
tatizo ni uagizaji wa Nondo zinazoingizwa Nchini kwa kulipiwa Ushuru
mdogo, naambiwa wa Asilimia 10 tu kama Kodi kwa visingizio mbalimbali na
hivyo kutoa ushindani usio halali kwa Nondo zinazozalishwa Nchini.
Aidha, mabati yanayoingizwa Nchini yamewekwa katika orodha ya “Deemed
Capital Goods” ambayo haiwabani watekelezaji wa Miradi mbalimbali nchini
kutumia mabati yanayotengenezwa na Viwanda vya Ndani.
Mheshimiwa Spika,
62. Tunavyo Viwanda vya kusindika Ngozi takriban tisa (9).
Viwanda hivi vina uwezo wa kusindika vipande vya Ngozi Milioni 13.2 kwa
mwaka katika hatua ya mwanzo yaani (Wet Blue). Kati ya hivyo vipande vya
ngozi za ng’ombe ni milioni 2.5 na vya mbuzi na kondoo ni Milioni 10.7.
Aidha, usindikaji wa ngozi ghafi umefikia Vipande 945,596 vya Ng’ombe
na Vipande 2,713,636 vya Mbuzi na Kondoo kwa mwaka 2013. Kama ilivyo kwa
Viwanda vya Chuma na Saruji, changamoto kubwa ya usindikaji wa ngozi ni
pamoja na ushindani usio wa haki unaosababishwa na uingizaji wa viatu
vya plastiki na mitumba ambao umeathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa
viatu vya Ngozi na bidhaa nyingine za Ngozi Nchini.
Mheshimiwa Spika,
63. Vilevile, tunalo tatizo kubwa katika Viwanda vya
uzalishaji wa Sukari Nchini. Tunavyo Viwanda takriban Vinne vya Sukari.
Uwezo wa uzalishaji Sukari Nchini ni Tani 300,000 kwa mwaka. Mahitaji ya
Sukari ni Tani 590,000 kwa mwaka (Tani 420,000 ni Sukari ya Matumizi ya
Kawaida na Tani 170,000 Sukari ya Matumizi ya Viwandani). Kwa maana
hiyo, kuna upungufu wa Tani 290,000 sawa na Asilimia 49. Kati ya hizo
Tani 170,000 (29%) ya Sukari ya matumizi ya Viwandani na Tani 120,0000
(20%) Sukari ya Matumizi ya Kawaida. Kutokana na upungufu huo, Serikali
iliweka utaratibu wa kuagiza na kusambaza Sukari kutoka Nje ya Nchi ili
kufidia pengo hilo kwa kuruhusu Waagizaji kulipa Ushuru wa Asilimia 25
na pia Ushuru wa Forodha Asilimia 10 kwa Viwanda vinavyotumia Sukari kwa
ajili ya matumizi ya Viwandani. Vipo pia vibali vya bila ushuru kabisa
vinavyotolewa wakati wa upungufu wa sukari.
Mheshimiwa Spika,
64. Utaratibu huu pamoja na kusimamiwa na Bodi ya Sukari
Tanzania (SBT), umesababisha malalamiko mengi kuwa hatua hizi za
kushusha Viwango vya Ushuru wa Forodha zimesababisha waingizaji Sukari
kukwepa kabisa Kodi, ikiwemo Ushuru wa Forodha na VAT. Aidha, zipo hisia
kuwa sukari hiyo ambayo ni nyingi zaidi ya kiasi kilichoruhusiwa
kuingizwa Nchini inatokana na Wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu
kutumia kinyume cha Sheria vibali vya Mamlaka ya Mapato Tanzania
vinavyowaruhusu kupitishia Nchini Sukari inayosafirishwa kwenda nje ya
Nchi (Transit Sugar) kwa kuibakiza bidhaa hiyo hapa Nchini na sukari ya
viwandani kuuzwa kama sukari ya mezani.
Mheshimiwa Spika,
65. Sukari hii inayoingizwa nchini huathiri uzalishaji na
mtiririko wa usambazaji sukari ya ndani hivyo kutishia ukuaji wa viwanda
vya ndani vya Sukari na uzalishaji wa sukari kwa ujumla. Vilevile,
itakumbukwa kuwa Serikali kwa nia njema, tulianzisha utaratibu wa
“Outgrowers” ili Wakulima wanaoishi kandokando ya Viwanda vya Sukari
kulima Miwa na kuuzia wenye Viwanda kule Kilombero, Mtibwa na Kagera ili
kuboresha maisha yao kiuchumi. Hivyo, kutokana na hali ilivyo kwa sasa,
Wakulima hawa wakiwemo Wakulima wa Kilombero wameshindwa kulipwa kwa
wakati baada ya kuuza Miwa yao Kiwandani kwa vile Wazalishaji wamekuwa
wakiuza Sukari chini ya Wastani wa mauzo ya kawaida.
Mheshimiwa Spika,
66. Nimeamua kuongea haya yote kuhusu hali halisi ya Viwanda
vyetu na bidhaa zinazozalishwa humu Nchini ili kuona umuhimu wa kujenga
Viwanda na changamoto tulizonazo katika kulinda Viwanda vyetu vya ndani
kwa kutumia mifano ya bidhaa za Chuma ikiwemo Mabati, Nondo, Saruji na
Sukari. Yapo mambo mengi ambayo yanajitokeza katika kila moja. Lakini
jambo la msingi ni namna ya kuangalia kama tunapokuwa na
mahitaji yanayozidi uwezo wa uzalishaji Viwandani tuchukue hatua
gani. Ni lazima kama Nchi pamoja na upungufu wa bidhaa uliopo, sasa
tuamue kulinda Viwanda vyetu vya ndani dhidi ya Ushindani usio halali
kwa nguvu zetu zote. Lazima sasa tukae tuone namna ya kudhibiti
uingizaji wa bidhaa ambazo zinakwamisha maendeleo ya Viwanda vyetu.
Aidha, tuangalie njia bora ya kupunguza gharama za uzalishaji, ikiwemo
bei kubwa za umeme. Matarajio ni kwamba, baada ya kupatikana kwa Gesi
tunaamini gharama za Umeme zitapungua na kupunguza gharama za uzalishaji
Viwandani.
Mheshimiwa Spika,
67. Tumeona changamoto zinazokabili bidhaa za Mabati, Nondo,
Sukari, Ngozi na Saruji kama mfano. Ninaagiza Taasisi zetu zikiwemo
Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Taasisi
za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),
Bodi ya Sukari, Jeshi la Polisi na Uhamiaji kukaa kwa pamoja kuangalia
njia bora ya kudhibiti uingizaji kiholela wa bidhaa zinazokwamisha
maendeleo ya Viwanda vyetu. Kwa maana hiyo ni vizuri sasa kuchukua hatua
stahiki kulinda Viwanda vyetu kuhimiza mambo muhimu yafuatayo:
i) Wizara ya Viwanda na
Biashara ni lazima sasa kuhakikisha kwamba Viwanda vyetu vinazalisha
bidhaa zenye ubora kwa Viwango vya Kimataifa. Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) lisaidie, lakini lazima ubora uwe unawezesha bidhaa hizo
kuuzwa ndani na nje bila vikwazo;
ii) Wizara ya Fedha ihakikishe
kuwa bidhaa zilizomo katika kundi la bidhaa nyeti katika Afrika
Mashariki haziondolewi katika kundi hilo katika kipindi kirefu kijacho
hadi hapo suala la Ruzuku likipatiwa ufumbuzi wenye manufaa kwa Nchi
changa katika Shirika la Biashara Duniani (WTO);
iii) Wizara ya Fedha iangalie
uwezekano wa watumiaji wa Industrial Sugar wanalipia Ushuru kamili na
kisha baadaye wapewe Duty Drawback baada ya kuthibitishwa kuwa Sukari
husika kweli ilitumika katika uzalishaji. Wizara ya Fedha pia iweke
utaratibu ulio bora wa uagizaji wa Sukari kufidia upungufu huu kutumia
Bulk Importation, na kisha kusambazwa kwa usimamizi madhubuti na kwa bei
maalum, n.k.;
iv) Wizara ya Kilimo, Chakula
na Ushirika na Bodi ya Sukari wakae na kutathmini mahitaji halisi ya
Sukari, ikilinganishwa na uwezo wa Viwanda vya Sukari vilivyopo Nchini,
pamoja na kukamilisha taratibu za kisheria na kimfumo za uagizaji wa
Sukari kuziba upungufu pale inapobidi. Aidha, ni muhimu kuhimiza upanuzi
katika uzalishaji wa Sukari kwa kuhamasisha Uwekezaji mpya katika Sekta
hii;
v) Utaratibu wa kuagiza bidhaa
zitakazoingizwa Nchini kuziba pengo lililopo lazima uangaliwe upya ili
uagizaji huo usiathiri Viwanda vya ndani;
vi) Tathmini ya upungufu wa
bidhaa unaojitokeza uangaliwe kwa umakini na kupanga njia bora ya
kufidia upungufu huo, ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa vibali vya
kuruhusu kuingiza bidhaa Nchini. Vibali vihusishe muda ule wenye
upungufu pekee. Aidha, utaratibu wa sasa wa kutumia Wafanyabiashara
kuleta bidhaa kwa lengo la kufidia upungufu wa bidhaa husika uangaliwe
upya ili kuepuka uingizaji bidhaa kwa wingi kuliko upungufu ambako
kunasababisha kudumaza Viwanda vya ndani; na
vii) Bei za bidhaa zizingatie
maeneo yanayozunguka eneo la Uzalishaji. Kwa mfano, haitarajiwi bei ya
Sukari kilo moja ya Sukari inayozalishwa na Kiwanda cha Sukari cha
Kagera au pale Moshi TPC, au Mtibwa na Kilombero iwe kubwa sawa na
Sukari hiyo inavyouzwa Mtwara au Ruvuma au Katavi.
Mheshimiwa Spika,
68. Ipo mifano kwa baadhi ya Nchi Duniani ikiwemo India
ambazo zimejaribu kuweka Nembo inayoonesha kwamba bidhaa hizi
zinazalishwa Nchini na bei yake ni kiasi fulani. Lengo likiwa ni
kuhakikisha kulinda watumiaji wa bidhaa hizo na kulinda pia Viwanda.
Majirani zetu Kenya wameanza kuchukua hatua katika Bajeti ya 2014
kulinda Viwanda vyao. Kwa mfano, Serikali ya Kenya imeongeza Ushuru wa
bidhaa za Chuma kutoka Asilimia 0-10 na kufikia Asilimia 25 na kuahidi
kuweka mezani Muswada mpya wa Sheria ya Ushuru wa Forodha ili kulinda
Viwanda vyake. Nasi tukidhamiria hata kama hatukufanikiwa kwa kiasi
kikubwa mwaka huu, tunaweza kufikia lengo hilo kwa mwaka ujao wa Bajeti.
Nina hakika Tukidhamiria tutaweza kufika!
UTOAJI WA ELIMU KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUMU NCHINI
Mheshimiwa Spika,
69. Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 inasisitiza kuhusu
haki ya kila raia wa Tanzania kupata Elimu wakiwemo watu Wenye Mahitaji
Maalumu; Sera ya maendeleo ya mtoto ya mwaka 1996 inayozungumzia
umuhimu wa kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule kwenda na kupata elimu
bora; na Sera ya Taifa ya Watu wenye Ulemavu ya 2004 – inasisitiza
umuhimu wa Elimu ya watoto wenye Ulemavu kutolewa katika mazingira
Jumuishi na rafiki. Katika kutekeleza Sera hizo, Serikali imekuwa
ikijitahidi kutoa elimu bora kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule,
wakiwemo wenye Mahitaji Maalumu.
Mheshimiwa Spika,
70. Kwa sasa zipo Shule za Msingi 22 ambazo ni maalum kwa
ajili ya Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum na Shule za Msingi 354 zenye
Vitengo Maalum kwa ajili ya Wanafunzi hao. Jumla ya Wanafunzi wenye
Mahitaji Maalum katika Shule za Msingi na Vitengo hivyo ni 11,689.
Aidha, ipo Shule moja ya Sekondari ambayo ni maalum kwa Wanafunzi wa
Sekondari wenye Mahitaji Maalum pamoja na Shule za Sekondari 61 ambazo
zina Vitengo Maalum kwa ajili ya Wanafunzi wa aina hiyo. Kwa sasa, wapo
Wanafunzi 1,406 wenye Mahitaji Maalum waliopo katika Shule za Sekondari
Nchini.
Mheshimiwa Spika,
71. Tarehe 3 Mei 2014 nilifungua maonesho ya Elimu
yaliyokuwa yameandaliwa na Wadau mbalimbali wa Elimu kwenye Uwanja wa
Jamhuri hapa Dodoma. Nilipata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali
yaliyokuwa yakionesha shughuli mbalimbali za elimu. Moja ya Banda
nililotembelea ni lile lililokuwa likionesha hatua mbalimbali za utoaji
wa elimu maalum. Katika Banda hilo nilielezwa njia zinazotumiwa
kuwafundisha Wanafunzi wenye Mahitaji maalum hususan Wasioona na
nilioneshwa vifaa vinavyotumika na kuelezwa changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Spika,
72. Tarehe 4 Juni 2014 nilitembelea na kukagua Shule ya
Msingi Bwigiri – Wasioona, Wilayani Chamwino. Katika ziara hiyo
nilikagua maktaba, chumba cha kompyuta, chumba cha kutayarishia mitihani
na vyoo. Niliongea pia na Wanafunzi waliokuwa wamebaki hapo shuleni
baada ya wanafunzi walio wengi kuwepo kwenye likizo. Shule hiyo ni
miongoni kwa Shule 120 za Msingi zilizoko kwenye Wilaya ya Chamwino
ikiwa na jumla ya Watumishi 39 kati yao 25 wakiwa ni Walimu. Shule ina
Wanafunzi 87, kati yao 61 ni Wasioona na 26 Wanaona. Jambo
lililonifurahisha katika Shule hiyo ni kuwa Wanafunzi wanaohitimu Darasa
la Saba wamekuwa wakifaulu wote (Asilimia 100) kwa muda wa miaka 13
mfululizo. Wanafunzi hao wanaofaulu wamekuwa wakijiunga na Shule Maalum
za Sekondari kama vile Shule ya Sekondari Diocese of Central Tanganyika
(DCT) Mvumi n.k.
Mheshimiwa Spika,
73. Tarehe 7 Juni 2014 nilitembelea pia Shule ya Sekondari ya
Mvumi DCT ambako baadhi ya Wanafunzi Wasioona wanasoma. Nilikutana na
Walimu pamoja na Wanafunzi wa Kidato cha Pili na Nne ambao walikuwa
wanajiandaa na mitihani ya Kitaifa ya mwaka 2014. Nilifurahishwa na kazi
kubwa inayofanywa na Serikali, Kanisa la Anglikana Nchini na Walimu wa
Shule hiyo kwa kuwawezesha Wanafunzi Wasiiona kupata haki yao ya elimu.
74. Ziara zangu hizo
zilinithibitishia kuwa Walimu Nchini wakiwemo Walimu wa Wanafunzi wenye
Mahitaji Maalum wanafanya kazi kubwa na ya Kizalendo ambayo inahitaji
kuungwa mkono wakati wote. Nawapongeza Walimu wote Nchini kwa kazi yao
muhimu ya kutoa elimu kwa Taifa letu. Nitumie fursa hii ya kipekee
kabisa kuwapongeza Walimu na Wanafunzi wote wa Shule ya Msingi Bwigiri –
Wasioona kwa kuwezesha mafanikio makubwa na ya kuigwa yaliyopatikana
Shuleni hapo. Aidha, nawapongeza Wasimamizi wa Elimu wa Mkoa wa Dodoma,
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI
kwa usimamizi wao mzuri uliowezesha ufaulu na mafanikio hayo kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
75. Pamoja na pongezi hizo, Ziara zangu hizo ziliniwezesha
kufahamu changamoto wanazokabiliana nazo Wanafunzi Wasioona wakiwa
shuleni. Ni kweli changamoto ni nyingi, lakini kubwa nililoliona na
ambalo limewagusa Wanafunzi hao pekee ni lile la Wanafunzi Wasioona
kutofundishwa somo la Hisabati katika ngazi ya Sekondari na hivyo,
kutofanya mtihani wa somo hilo wa kumaliza Kidato cha Nne na kusababisha
kushushwa madaraja yao ya ufaulu sawa na Wanafunzi wa kawaida katika
Shule zingine Nchini wasiofaulu somo hilo. Lakini Shule hizi zinakosa
vitendea kazi muhimu kama vile Braille Printer, Embossing Photocopy
Machine, Kompyuta, n.k.
Mheshimiwa Spika,
76. Ninafahamu kuwa changamoto nyingine si za Wanafunzi
wasioona tu bali zinawahusu pia Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum pamoja
na Walimu wao kwa ujumla. Napenda kutoa wito kwa Watendaji wanaohusika
na elimu maalum Nchini kushughulikia changamoto zonazowakabili Walimu na
Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum pamoja na Majengo ya Shule zao. Ni
imani yangu kuwa kila mmoja anayehusika atachukua hatua mapema ili
kuwawezesha Wanafunzi Wasioona na wote Wenye Mahitaji Maalum kupata
elimu stahiki katika mazingira stahiki.
AFYA
Uwiano wa Idadi ya Watu wa Vijijini na Mijini wanaohudumiwa na Daktari
Mheshimiwa Spika,
77. Idadi ya Watanzania inakadiriwa kuwa Milioni 48.2 kati
yao wanaoishi Vijijini ni Milioni 36.6 na wanaoishi Mijini ni Milioni
11.6. Watanzania hao wanahudumiwa na Madaktari ni 2,311 waliopo Nchini
kwa sasa. Madaktari wanaoishi maeneo ya Vijijini ni 523 na wanaoishi
maeneo ya Mijini ni 1,788. Mgawanyo huu wa Madaktari unafanya kuwa
Daktari mmoja kitaifa anahudumia Wastani wa Watanzania 19,982. Kwa
upande wa Vijijini, Daktari mmoja anahudumia Wananchi 66,211 wanaoishi
Vijijini na kwa maeneo ya Mijini, Daktari mmoja anahudumia Wananchi
6,460. Hali hii inaonesha kuwa Daktari mmoja anayehudumia maeneo ya
Vijijini anahudumia zaidi ya mara kumi ya idadi ya watu wanaohudumiwa na
Daktari anayefanya kazi Mjini.
78. Kiwango hiki cha Daktari
mmoja kwa Watanzania 19,982 ni kikubwa sana ikilinganishwa na wastani wa
kawaida wa Daktari mmoja kwa Watu 10,000. Kinahitaji kupunguzwa kwa
kuongeza idadi ya Madaktari Nchini. Serikali itaendelea kugharamia elimu
ya Madaktari Nchini na kuwawezesha kuwa na mazingira bora ya kazi kwa
kuzingatia hali ya uchumi wa Nchi. Nia ni kuongeza idadi ya Madaktari wa
ngazi na vitengo mbalimbali vya Afya na kuwasambaza Nchini hususan
maeneo ya Vijijini ili Daktari mmoja ahudumie Watanzania wachache zaidi.
Saratani ya Shingo ya Kizazi
Mheshimiwa Spika,
79. Serikali imeanzisha mpango wa kitaifa wa kukinga na
kuzuia saratani ya shingo ya kizazi. Aidha, Serikali itaendelea kutoa
elimu kuhusu kujikinga na saratani ya awali, kupanua vituo vya kupima
dalili za awali za saratani na kupatiwa tiba ya ugandishaji baridi
kwenye Mikoa mitatu iliyobakia ya Mtwara, Rukwa na Simiyu. Huduma ya
rufaa itaboreshwa kwa wagonjwa wanaofikiriwa kuwa na saratani kwa ajili
ya tiba katika Taasisi ya Saratani ya Dar-es-Salaam. Aidha, chanjo ya
kuwakinga Wasichana wenye umri wa miaka 9-13 dhidi ya saratani imeanza
kutolewa katika Mkoa wa Kilimanjaro ili kujifunza mfumo wa kutumia Shule
kwa ajili ya kutoa chanjo hii nchi nzima.
HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
80. Kwa ujumla hali ya usalama katika Mipaka yote ya Nchi
yetu inaendelea kuwa shwari licha ya kuwepo changamoto kadhaa.
Mathalani katika Mpaka wa Kaskazini ambapo Tanzania inapakana na Kenya
na Uganda kumekuwepo na changamoto ya Wahamiaji haramu hususan katika
Wilaya za Misenyi na Karagwe na changamoto ya uharibifu wa alama za
Mipaka. Aidha, katika Mpaka wa Kusini pamekuwepo na changamoto ya utata
wa Mpaka kati ya Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa na changamoto ya
ujenzi holela unaofanywa na Wananchi waishio Mpakani eneo la Tunduma.
Mheshimiwa Spika,
81. Serikali kupitia Vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inaendelea kuchukua
hatua mbalimbali za kudhibiti hali hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya
mazungumzo ya pamoja baina ya Wataalamu wetu na Wataalamu wa Nchi hizo
jirani kwa mfano:
i) Tarehe 05 hadi 12 Octoba,
2013 Mjini Arusha vilifanyika Vikao vya pamoja kukagua, na kuhakiki
Mpaka kati ya Tanzania na Kenya;
ii) Mwezi Februari 2014 Jijini
Dar es Salaam kilifanyika kikao cha kuboresha Mipaka ya Tanzania,
Burundi, Zambia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika ziwa
Tanganyika;
iii) Mwezi Mei, 2014 kilifanyika Kikao cha TUME ya Uimarishaji na Uhakiki wa Mpaka baina ya Tanzania na Burundi Mjini Ngara.
Mheshimiwa Spika,
82. Pamoja na kwamba kwa ujumla hali ya usalama wa Mipaka
yetu ni shwari, bado Nchi yetu kama sehemu ya Afrika Mashariki
inakabiliwa na tishio la mashambulizi ya Kigaidi ambalo linawakumba
Majirani zetu. Serikali kupitia Jeshi la Wananchi Tanzania inaendelea
kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Nchi jirani, Nchi
Marafiki pamoja na Jumuia ya Kimataifa ili kukabili tishio hilo. Nitoe
wito tena kwa Wananchi wetu kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Vyombo vya
Usalama katika kuhakikisha Nchi yetu inakuwa salama wakati wote.
AJALI ZA BARABARANI
Mheshimiwa Spika,
83. Suala la ajali za barabarani bado ni changamoto kubwa
hapa Nchini likichangia vifo na majeruhi wengi na uharibifu wa mali.
Pamoja na hatua mbalimbali za kisheria, bado kumekuwa na ongezeko la
ajali za barabarani mwaka hadi mwaka. Katika kipindi cha Januari 2011
hadi Mei 2014, jumla ya Ajali 78,654 ambazo zilisababisha Vifo 13,375 na
Majeruhi 67,936 zilitokea. Hii ni idadi kubwa ya ajali, vifo na
majeruhi.
Mheshimiwa Spika,
84. Ziko sababu mbalimbali zinazochangia kuongezeka kwa ajali
za barabarani zikiwemo makosa ya kibinadamu (Uzembe wa Madereva, Ulevi,
Mwendokasi na Uegeshaji mbaya wa magari barabarani n.k.) ambayo kwa
ujumla yanachangia Asilimia 77 ya ajali zote zinazotokea, ubovu wa
vyombo vya moto unaochangia Asilimia 16, na mazingira ya barabara yaani
ubovu wa miundombinu na hali ya hewa vinavyochangia Asilimia 7.
Mheshimiwa Spika,
85. Katika kukabiliana na ajali za barabarani, Serikali
kupitia Vyombo mbalimbali imechukua hatua za kuimarisha mafunzo kwa
Madereva kwa kutunga Kanuni zinazowalazimisha kusoma masomo ya umahiri
wa kuendesha magari ya abiria na magari makubwa ya mizigo (HDV);
kudhibiti mwendokasi na kuanzisha Mfumo wa kufuatilia mwendo wa Mabasi
na Malori utakaodhibiti makosa mbalimbali ya usalama barabarani. Hatua
nyingine ni kuanzisha mfumo wa uwekaji nukta (Point system) katika
Leseni za Madereva ili kuwaondoa barabarani madereva wanaokithiri kwa
makosa, kupima kiasi cha ulevi kwa Madereva; na kupanua wigo wa elimu ya
usalama barabarani kwa njia ya televisheni, redio, simu na magazeti.
Kwa upande wa Usimamizi wa Sheria zilizopo, hatua stahiki zinachukuliwa
kwa kuongeza usimamizi na mafunzo kwa watendaji wote wanaosimamia Sheria
ili kuwaongezea ufanisi na kudhibiti nidhamu yao. Watendaji wanaokiuka
maadili ya kazi wanachukuliwa hatua za kinidhamu.
Mheshimiwa Spika,
86. Kwa upande wa ubovu wa vyombo vya moto, Serikali inaandaa
Kanuni za Ukaguzi wa Lazima. Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)
kimekamilisha ujenzi wa mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa magari ikiwa ni
pamoja na mitambo ya kukabiliana na uchafuzi wa hewa. Ninatoa wito pia
kwa Sekta Binafsi kujitokeza kuwekeza katika eneo hili ili mitambo hii
iwepo ya kutosha. Aidha ni muhimu sasa kuanzisha Gereji maalum kwa ajili
ya matengenezo yatakayokuwa yanapimwa kwa mfumo huu. Sambamba na hatua
hizo, Jeshi la Polisi pia linaandaa Kanuni zitakazowalazimu Madereva
kubandika mkanda ang’avu kuzunguka magari makubwa ya mizigo na mabasi
ili kusaidia kuongeza muonekano wa magari hayo wakati wa giza.
Mheshimiwa Spika,
87. Pamoja na jitihada hizo za Serikali za kuandaa Kanuni
mbalimbali, Sheria mpya ya Usalama Barabarani inaweka muundo bora wa
usimamizi wa shughuli za Usalama barabarani kwa kuweka hitaji la kuundwa
kwa Taasisi Kiongozi ya Usalama Barabarani (Road Safety Lead Agency).
Sheria hiyo itaanisha majukumu ya Taasisi Wadau wa Usalama Barabarani na
kuratibu utekelezwaji wa majukumu ya Taasisi hizo. Uwepo wa Chombo hiki
utaongeza uwajibikaji wa kila Taasisi katika eneo lake tofauti na sasa
ambapo suala la usalama barabarani linachukuliwa kama jukumu la Polisi
pekee. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Taasisi na Wadau mbalimbali
wanafanya mapitio ya rasimu ya Muswada huu ambao mara utakapokamilika
utawasilishwa Bungeni.
MAUAJI YA WALEMAVU WA NGOZI NA VIKONGWE
Mheshimiwa Spika,
88. Nchi yetu bado inaendelea kukumbwa na tatizo la Mauaji ya
Watu wenye Ulemevu wa Ngozi na Vikongwe kwa imani za ushirikina. Katika
kipindi cha mwaka 2012 hadi 2014, takwimu zinaonesha kwamba jumla ya
Watu 3 wenye Ulemavu wa Ngozi waliuawa katika Mikoa ya Arusha, Tabora na
Simiyu na wengine 2 walijeruhiwa katika Mkoa wa Rukwa. Kufuatia matukio
hayo, watuhumiwa 8 wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani kwa mauaji na
wengine 4 wanashtakiwa kwa kujeruhi. Aidha, katika kipindi hicho jumla
ya Vikongwe 1,393 waliuawa kikatili katika Mikoa ya Geita, Shinyanga,
Mara, Simiyu, Mwanza, Tabora, Singida, Mbeya, Iringa, Njombe na Rukwa.
Mheshimiwa Spika,
89. Kwa kutambua ukubwa wa tatizo hili, Serikali inachukua
hatua ya kuzihusisha Kamati za Ulinzi na Usalama za ngazi mbalimbali
kuanzia Vitongoji na Mitaa katika mapambano dhidi ya mauaji ya Vikongwe
kwa kufanya Mauaji ya Watu wenye Ulemavu na Vikongwe kuwa Agenda ya
kudumu katika Mikutano yao. Aidha, tutaendelea kutoa elimu kwa Wananchi
kupitia Vyombo vya Habari, Viongozi wa Dini na Watu mashuhuri katika
maeneo husika ya kuepukana na imani potofu za ushirikina. Jeshi la
Polisi linaendesha Program mbalimbali kuelimisha Jamii kukabiliana na
uhalifu kufanya ufuatiliaji wa matukio ya mauaji ya Vikongwe ikiwa ni
pamoja na kuweka mkakati wa kuharakisha upelelezi wa kesi za matukio ya
Mauaji.
MAUAJI YA WANAWAKE MKOANI MARA
Mheshimiwa Spika,
90. Pamoja na Mauaji ya Vikongwe na Watu wenye Ulemavu wa Ngozi katika Mkoa wa Mara kumetokea mauaji ya kinyama ya Wanawake kutokana na sababu za kishirikina katika kipindi cha Januari hadi Mei 2014 hususan katika Wilaya za Butiama na Musoma. Waathirika wa matukio haya walikuwa wakiuawa kwa kunyongwa kwa kutumia khanga nyakati za mchana wakiwa katika shughuli zao na hivyo kusababisha hofu kubwa katika Jamii. Jumla ya matukio tisa (9) ya kuuawa Wanawake yaliripotiwa katika Kata nne za Mugangwa, Etaro, Nyegina na Nyakatende.
Mheshimiwa Spika,
91. Kufuatia matukio hayo Serikali kupitia Jeshi la Polisi na
kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imechukua hatua
za haraka na jumla ya watuhumiwa 15 wamekamatwa na kufikishwa
Mahakamani kwa kesi za mauaji. Aidha, Kikosi Kazi cha Makosa dhidi ya
Binadamu na vitendea kazi kutoka Makao Makuu ya Upelelezi kikiongozwa na
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania Kamishna ISAYA
MNGULU walifika Mkoani Mara kwa ajili ya ufuatilia wa karibu wa
kitaalamu wa matukio haya. Timu hiyo wenye Wataalam mahiri katika eneo
la Upelelezi wanaendelea kufuatilia matukio haya sambamba na kutoa
elimu juu ya Ulinzi Shirikishi wa namna ya kukabiliana na matukio
kama haya,ikiwa ni pamoja na kutoa elimu zaidi kuhusu uhalifu huu na
kufanaya Operesheni ijulikanayo kama “Zuia Mauaji ya akina Mama Wilaya
ya Butiama.”
Mheshimiwa Spika,
92. Kutokana na juhudi hizo, hali ya Usalama katika maeneo
hayo imeimarika na matukio hayo hayajajitokeza tena. Napenda kutoa wito
kwa Wananchi wote kutambua kuwa jukumu la ulinzi ni la kila Mwananchi,
hivyo hatuna budi kuwafichua wale wote wanaofanya uhalifu katika Jamii.
Lengo ni kuwalinda Wananchi na kuhakikisha kuwa maeneo tunayoishi
yanakuwa na ulinzi na usalama wa kutosha ili Wananchi waendelee na
shughuli zao za uzalishaji badala ya kuhofia maisha yao.
MCHAKATO WA KATIBA MPYA NA MUSTAKABALI WA TAIFA
Mheshimiwa Spika,
93. Kama wote tunavyofahamu, Bunge Maalum la Katiba liliaanza
majukumu yake mapema mwezi Februari 2014 ambapo katika kipindi hicho
Wajumbe walikamilisha kuandika na kupitisha Kanuni za Bunge Maalum la
Katiba, kufanya uchaguzi wa Viongozi wa Bunge Maalum, Wajumbe kujadili
Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba hiyo na Kamati za Bunge
Maalum kuwasilisha maoni yao Bungeni. Hata hivyo, na kwa masikitiko
makubwa wakati tukiwa katika hatua za uwasilishaji, baadhi ya Wajumbe
wanaounda Umoja wa Katiba na Wananchi (UKAWA) waliamua kutoka nje ya
Bunge kwa sababu ambazo hazikueleweka wakati huo.
Mheshimiwa Spika,
94. Wote tunafahamu kuwa, Bunge Maalum la Katiba lina
Wajumbe wa aina tatu wakiwemo Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi
na Wajumbe 201 wanaotoka katika Makundi mbalimbali. Kwa kuwa Waheshimiwa
Wabunge wote wa Bunge hili ni sehemu ya Wajumbe wa Bunge Maalum, naomba
nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kutoa ujumbe mfupi kwa
Wajumbe wa Bunge Maalum ambao naamini utaweza kuwafikia popote walipo.
Mheshimiwa Spika,
95. Kifungu cha 26 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
kinatoa masharti na mamlaka ya Bunge Maalum kutunga Kanuni kwa ajili ya
kuendesha shughuli za Bunge Maalum. Ni kwa kupitia mamlaka kama
ilivyofafanuliwa katika Kifungu hiki, Wabunge wa Bunge Maalum waliweza
kutunga Kanuni za Bunge Maalum kwa maridhiano kwa muda wa
takriban mwezi mmoja. Vilevile, ni kupitia Kanuni hizo, Viongozi wa
Bunge Maalum waliweza kuchaguliwa na kufanya Bunge hilo kuwa Chombo
Maalum chenye Uongozi na kuwa na Mamlaka yake ya Kisheria.
Mheshimiwa Spika,
96. Kanuni ya 46 ya Bunge Maalum la Katiba inaeleza mambo
yasiyoruhusiwa kwenye Bunge Maalum yakiwemo kutumia lugha ya kuudhi,
kubagua, kunyanyapaa au inayodhalilisha watu wengine. Aidha, Kanuni hii
ya 46 inatoa utaratibu mzima wa jinsi ya kushughulikia masuala haya
ndani ya Bunge Maalum. Kanuni ya 16 (3) inatoa nafasi kwa Mjumbe au
Wajumbe wa Bunge hilo ambaye hakuridhika na uamuzi wa Mwenyekiti
uliotolewa, kuwa atakuwa na haki ya kuwasilisha kwa maandishi malalamiko
yake kwa Katibu ndani ya siku moja kuanzia tarehe ya uamuzi.
97. Kwa muendelezo huo huo,
Kanuni ya 59 (1) (d) inaelekeza kuwa, moja ya majukumu ya Kamati ya
Kanuni na Haki za Bunge Maalum ni kuchunguza kuhusu masuala yote ya
haki, kinga na madaraka ya Bunge Maalum yatakayopelekwa kwenye Kamati
hiyo na Katibu kutoa taarifa kwa Mwenyekiti baada ya taarifa hiyo
kuwasilishwa kwenye Bunge Maalum.
Kutokana na utaratibu huo wa Kikanuni
kama ilivyoainishwa katika Kanuni hizo za Bunge Maalum, ninapenda
kutumia fursa hii kuwashauri “Wana UKAWA” ambao wengi wao wamo ndani ya
Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wenzangu wote
wa Bunge Maalum ambao wamo ndani na nje ya Bunge hili la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa ujumla wetu kutumia mifumo iliyowekwa na Bunge
Maalum kupeleka malalamiko yote katika Kamati ya Kanuni ya Bunge Maalum
ili yapatiwe ufumbuzi ndani ya Bunge Maalum na siyo nje ya Bunge. Hilo
ndilo jambo la busara!!
Mheshimiwa Spika,
98. Mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya, ambao kimsingi ni
wa Kisheria umeanza siku nyingi na kwa hatua mbalimbali shirikishi kwa
makundi ya watu na Vyombo mbalimbali, kupokezana majukumu kwa lengo la
kufanikisha azma ya kupata Katiba Mpya. Ninapenda kuwakumbusha Wajumbe
wenzangu wa Bunge Maalum la Katiba popote walipo ndani na nje ya Bunge
hili kuwa, kuwepo kwetu katika Bunge Maalum la Katiba ni jambo la
Kisheria na si jambo la kawaida wala la hiari. Wajumbe wa Bunge Maalum
la Katiba, sote kwa ujumla wetu tuna wajibu wa kukamilisha sehemu yetu
kama Wajumbe wa Bunge Maalum kwenye mchakato mzima wa kuandaa Katiba
Mpya.
Mheshimiwa Spika,
99. Vilevile, napenda kukumbusha kuwa Bunge Maalum la Katiba
si hatua ya mwisho ya mchakato huu. Baada ya Bunge Maalum la Katiba
kumaliza wajibu wake, Rasimu itakayokuwa imependekezwa na Bunge Maalum
itatakiwa kuwasilishwa kwa Wananchi wote wa Tanzania waisome, waielewe
na kisha waweze kuipigia kura ya maoni kuikubali au kuikataa kwa mujibu
wa Sheria iliyopo ya Kura ya Maoni mwaka 2013. Hivyo, ni vyema tukaelewa
vizuri suala hili na kwamba, bado kuna Wananchi wenzetu wengi kwa idadi
ambao nao wanasubiri haki yao ya Kisheria katika kukamilisha mchakato
huu kabla ya kupata Katiba Mpya. Hivyo tusiwanyime haki hiyo!
100. Ninapenda kuwashauri
Wajumbe wenzangu ambao wameamua kususia Vikao vya Bunge Maalum la Katiba
kutafakari uamuzi na matendo yao kwa kutambua masharti ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalum la Katiba na wajibu wao
kwa Wananchi. Sisi wote tuliopo hapa tuna wajibu huo wa kukamilisha kazi
hii muhimu tuliyopewa kisheria ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata
Katiba Mpya.
101. Hivyo, natoa wito kwa
Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba ambao wamesusia Vikao vya Bunge
Maalum la Katiba, warejee kwenye Bunge hilo ili tuweze kuendelea na
Mjadala wa Rasimu ya Katiba huku tukitumia utaratibu mzuri wa maridhiano
uliowekwa Kikanuni kutatua tofauti zilizopo.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
102. Changamoto kubwa iliyoko mbele yetu baada ya kuwepo hapa
Bungeni kwa takriban miezi miwili ni kusimamia utekelezaji wa Bajeti ya
Serikali tuliyoipitisha. Sisi kama Wabunge tuondoke hapa kwa lengo moja
la kushirikiana na Wananchi kusukuma maendeleo na Bajeti tuliyoipitisha
ikiwa ndiyo kichocheo kikuu. Twendeni tukasisitize umuhimu wa kuishi
kwa amani, upendo na mshikamano. Tukiwasimamia vizuri na kuwaongoza
Wananchi katika matumizi ya rasilimali hata kama ni kidogo kiasi gani,
Nchi yetu itasonga mbele kimaendeleo na maisha bora kwa Wananchi wetu
yatapatikana.
SHUKRANI
Mheshimiwa Spika,
103. Baada ya kusema hayo, napenda hasa nimalizie kwa
kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Nikushukuru kwa
namna ya pekee wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa
kutuongoza vizuri kulingana na Kanuni za Bunge. Aidha, nimshukuru
Mwenyekiti, Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala kwa kuongoza
vizuri baadhi ya Vikao vya Bunge wakati wa Mkutano huu. Ninawashukuru
tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu ya dhati na yenye
Mantiki kwa ajili ya Maendeleo ya Nchi yetu. Niwashukuru Waheshimiwa
Mawaziri, Naibu Mawaziri, Watumishi na Wataalam wote wa Serikali
waliosaidia kujibu Maswali na hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge na
mambo mengine yanayohusiana na Bajeti hii. Vilevile, nawashukuru
Waandishi wa Vyombo vya Habari kwa kuwapatia Wananchi habari kuhusu
Majadiliano yaliyokuwa yanaendelea hapa Bungeni. Wote kwa ujumla wenu
nawashukuru sana.
Mheshimiwa Spika,
104. Kipekee napenda kuwashukuru Madereva wote ambao wamekuwa
makini katika kazi ya kuwaendesha Viongozi wote, wakiwemo Waheshimiwa
Wabunge na Wataalam kutoka shemu mbalimbali Nchini na kuwawezesha kufika
hapa Dodoma kuhudhuria Mkutano huu wa Kumi na Tano. Vilevile,
nawashukuru Wananchi wa Mkoa wa Dodoma, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa,
Mheshimiwa Dkt. Rehema Nchimbi kwa ukarimu wao kwa muda wote tuliokaa
hapa Dodoma. Nivishukuru pia Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambavyo
vimehakikisha muda wote tumekaa kwa Amani na Utulivu mkubwa. Mwisho
namshukuru Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilillah na Watumishi wote wa
Ofisi ya Bunge kwa huduma nzuri zilizowezesha kukamilisha shughuli
zilizopangwa katika Mkutano huu bila matatizo.
Mheshimiwa Spika,
105. Nitumie fursa hii kuwaombea safari njema mnaporudi
katika maeneo yenu ya kazi. Lakini pia niwaombee kheri na
Baraka tele Waislamu wote ambao wameanza na wanaendelea na Mfungo wa
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kila atakayeamua kufanya Ibada hiyo aifanye
kikamilifu na kama Kitabu cha Quran Tukufu kinavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika,
106. Baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kwamba, Bunge
lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 04 Novemba, 2014 siku ya
Jumanne, Saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 16 kwenye
Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa Spika,
107. Naomba kutoa hoja
No comments:
Post a Comment