Baadhi ya viongozi na wadau wa
elimu mkoani Pwani wakimsikiliza mkuu wa mkoa huo mhandisi Evarist
Ndikilo ,wakati alipokuwa akizungumza masuala ya elimu na changamoto
zinaxokabili sekta hiyo ,kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi
ya mkuu wa mkoa wa Pwani
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi
Evarist Ndikilo, akizungumza jambo kuhusu masuala ya sekta ya elimu na
changamoto inazozikabili kwa viongozi na wadau mbalimbali wa elimu
mkoani hapo kwenye ukumbi wa mikutano katika ofisi za jengo la mkuu wa
mkoa .
Picha na Mwamvua Mwinyi
…………..
Na Nurudini stambuli,Pwani
SERIKALI mkoani Pwani
,imeweka bayana kuwa,jumla ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
1,300 wameacha shule (mdondoko),kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia
2014-2017,hali inayosababisha kukosa haki yao ya elimu.
Aidha kumekuwa na
tetesi kwamba baadhi ya watoto hao wanaoacha shule hujihusisha na
vikundi vya uhalifu ndani na nje ya mkoa huo ,jambo ambalo linahitaji
nguvu za pamoja kulikomesha tatizo hilo.
Pamoja na hilo
,imeeleza kumekuwepo na tatizo la uzembe kwa baadhi ya wasimamizi wa
elimu kutotekeleza ipasavyo majukumu yao,;:na pia kutofikiwa kwa malengo
ya uandikishaji wa elimu ya awali na darasa la kwanza na udahili wa
kidato cha kwanza hivyo kusababisha watoto wenye umri wa kwenda shule
kutokwenda shule.
Mkuu wa Mkoa wa
Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,aliyasema hayo wakati akizungumzia
changamoto na masuala ya sekta ya elimu mkoa,kwa viongozi wa Idara ya
elimu mkoani hapo, wakurugenzi,wakuu wa wilaya na wadau wa elimu.
Alielezea ,kati ya
watoto hao 1,300 wanaodaiwa kuacha shule kwenye mkoa mzima ,kwa upande
wa wilaya ya Rufiji ni wanafunzi 381 na Kibiti ni 110 .
“Niliwahi kuomba taarifa ya mdondoko kwa kipindi cha mwaka 2014-2017 kutoka kwa wakuu wa wilaya zote “
“Ambapo mkoa wa Pwani
una jumla ya shule za msingi 613 na sekondari 174 ,ndipo nilipoletewa
idadi hiyo ambayo kiukweli ni chanzo cha kuporomoko kwa taaluma mkoani
hapo” alisema mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo
aliagiza wanafunzi wote walioacha shule na watoro watafutwe ,warudishwe
shule kisha wazazi na walezi wachukuliwe hatua za kisheria ikiwepo
kufikishwa mahakamani kwa kushindwa kufuatilia mahudhurio ya watoto hao.
Alibainisha lipo
tatizo jingine la mimba kwa watoto wa kike ,upungufu na uchakavu wa
miundombinu ya shule ikiwemo madarasa ,nyumba za walimu ,matundu ya
vyoo,ofisi za walimu, maabara na hostel.
Mkuu huyo wa mkoa,
alisema kwasasa shule za msingi kuna mahitaji ya vyumba vya madarasa
7,609 ,vilivyopo ni 4,010 hivyo upungufu ni madarasa 3,599.
Mahitaji ya nyumba za
walimu ni 6,328 ,zilizopo ni 1,592 ,upungufu ni nyumba 4,736 ,matundu
ya vyoo yanayohitajika ni 13,750 ,yaliyopo ni 5,375 upungufu ni matundu
8,375 .
Mhandisi Ndikilo
alitaja mahitaji ya vyumba vya madarasa katika shule za sekondari mkoani
Pwani kuwa ni 1,479 ,vilivyopo ni 1,366 ,upungufu ni 113 ,mahitaji ya
nyumba za walimu 3,684 zilizopo 671 hivyo upungufu 3,013.
Matundu ya vyoo
yanayohitajika ni 2,405 yaliyopo ni matundu 1,961,upungufu ni matundu
444 ,na mahitaji ya maabara ni 333 yaliyopo ni 195 na upungufu ni 138.
Hata hivyo ,Mhandisi
Ndikilo alizitaka halmashauri mkoani humo ,ziande mkakati wa kujenga
hostel katika kila shule ya sekondari ili kuwalinda watoto hasa wa kike
wanaotembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule.
Sanjali na hilo ,ziwe
na mpango mkakati wa kujenga na kukarabati miundombinu ya shule ikiwemo
vyumba vya madarasa ,matundu ya vyoo na nyumba za walimu na kukamilisha
ujenzi ifikapo 2020 .
Alitoa wito kwa wadau
wa elimu kuunga mkono juhudi za serikali ya mkoa katika ujenzi wa
miundombinu katika shule za msingi na sekondari.
Katika hatua nyingine
,mhandisi Ndikilo alisema lengo la serikali ni kuimarisha sera ya
viwanda ili kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 ,na msingi mkubwa wa
sera hiyo ni elimu.
Aliwataka wakuu wa
wilaya, wakurugenzi, watendaji wa halmashauri pamoja na watendaji
wengine kuhakikisha wanafunzi wanaodahiliwa kidato cha kwanza
wanasimamiwa hadi wanamaliza kidato cha nne ili waweze kushiriki katika
kuimarisha uchumi wa viwanda.
Alisema kwamba,watoto
wasipopewa elimu ,maarifa na ujuzi mahsusi watakuwa watazamaji badala
ya watendaji licha ya mkoa huo kusheheni viwanda.
No comments:
Post a Comment