
Kichwani mwangu nasikia kelele nyingi za wabunge wakiongozwa na Mhe. James Mbatia kuhusu udhibiti wa vitabu vinavyotumika shuleni, lakini machoni naona wazi kabisa kuwa watendaji wa vyombo husika hawasikii kilio kile cha wawakilishi wa wananchi bungeni.
Bila shaka tulio wengi tunakumbuka kuwa Juni mwaka jana, Mbatia ambaye ni mbunge wa kuteuliwa na rais, aliweka bayana udhaifu mwingi aliougundua kuwemo katika vitabu vilivyoidhinishwa na iliyokuwa Kamati ya Ithibati ya Vifaa vya Elimu (EMAC).
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi alilia na kilio chake kikaungwa mkono na wabunge wengi wakadhani kuwa uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi umesikia na ukaamua kuivunja EMAC, lakini madudu zaidi yamebainika kwenye vitabu vilivyonunuliwa kwa fedha za fidia ya rada na kusambazwa mashuleni.
Mwaka jana, serikali ilitangaza kuwa fedha hizo ambazo ni pauni milioni 29.5 za Kiingereza (sawa na Shilingi bilioni 73.6 ), zililengwa kwa ajili ya ununuzi wa vitabu vya kiada, mihutasari ya elimu ya msingi na madawati.
Ukiondoa mgawanyo wa vitabu hivyo ambavyo haukuzingatia mahitaji kwa shule, walimu katika maeneo mbalimbali nchini wanalalamika kuwa vitabu vingi vina makosa ya maarifa na uchapaji, licha ya kuwa vilipata ithibati kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wanatoa mifano kuwa kitabu kimoja cha hisabati darasa la saba, kuna tofauti ya majibu ya maswali namba 7 na 12 kama yalivyo katika kitabu chake cha Kiongozi cha Mwalimu. Swali la 7 (-17 ×-13) ambalo jibu lilipaswa kuwa +221, mwandishi ameweka jibu la + 909903391 ambalo ni jibu la swali la 12 linalosema: -31375979× -29
Katika kitabu hichohicho, kuna swali linalosema; Tafuta kipeuo cha pili cha 102 - 62 , badala jibu kuwa 8 mwandishi ameandika 20.
Mfano mwingine wanaoutoa walimu wanaofundisha watoto wetu ni katika mada ya Ubongo wa Nyuma (serebelamu), kitabu kimoja kinasema serebelamu huhusika na matendo yasiyo ya hiari huku kitabu kingine kikielezea kuwa serebelamu inahusika na uratibu wa matendo ya hiari.
Kasoro nyingine imejitokeza katika tofauti ya majina na idadi ya aina za misuli. Kitabu kimoja kinaaandika kuwa kuna aina kuu mbili za misuli katika mwili wa binadamu ambazo ni misuli ya hiari na misuli isiyo ya hiari huku kingine kikisema kuna misuli mikuu ya aina tatu ambayo ni misuli myoyoro, misuli ya moyo na misuli ya mfumo wa mifupa.
Kitabu kingine cha Kiswahili, mwandishi amekosa mtiririko wa kiuandishi hivyo kuwakanganya walimu na wanafunzi wanaokisoma. Katika kitabu hicho mada ya Aina za Maneno iliyoanza ukurasa wa 10 na aina ya kwanza ‘Nomino’ badala ya kuendelea na mada hiyo kwa mfuatano wa kurasa, aina nyingine na maneno zinaonyeshwa kutajwa ukurasa wa 85 na 118.
Wasomi hawakufumbia macho haya kwani Dk. George Kahangwa, mtaalamu wa fani ya elimu na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amekaririwa akisema kuwa mambo hayo ni aibu kwa taifa.
Hakumung’unya maneno amesema haya ni miongoni mwa mambo yanayoliaibisha taifa letu na kulitengenezea kifo cha taratibu.
Itakumbukwa kwamba hii si mara ya kwanza tunasikia uwepo wa aibu hii ya vitabu vibovu. Mwaka jana, Taasisi ya EMAC ilishutumiwa na baadhi ya wabunge kwa kutoa ithibati kwa vitabu visivyo na viwango, hadi serikali ikaamua kuifuta taasisi hiyo.
Naamini kwamba kama taifa, tumefika hapa si kwa sababu tu ya rushwa bali mzizi wa tatizo ni watu kukosa uzalendo, umakini na uelewa wa wanachokifanya, hasa wale tuliowapa dhamana ya kuhakikisha elimu inasonga mbele.
Ofisa mwenye uzalendo hawezi kutanguliza masilahi yake ya kupata chochote na kupitisha vitabu vyenye kasoro za watu kuingia darasani na kuonekana vingi ni shaghalabaghala na kuacha vikiua elimu katika taifa lake.
Kukosa uzalendo ndiyo kunakofanya elimu inafifia na hata kwenye kuingiza vyakula wasio wazalendo wapo radhi kuingiza chakula huku wakijua hakifai kuliwa na watu.
Kukosa uzalendo, upendeleo, ubinafsi na kujitajirisha kwa njia ya mkato huku kazi ambazo zinahitaji ujuzi wakipewa wasio na ujuzi katika fani husika matokeo yake huwa ni kuua taifa.
Nishauri na kusema kwamba serikali inao wajibu wa kufanya kazi zake kwa uangalifu mkubwa kuondoa kasoro hizi ambazo zinaua elimu.
Serikali inapaswa kuwashughulikia wahusika katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na idara nyinginezo zilizohusika katika hili la vitabu maana wameitia aibu dola.
No comments:
Post a Comment