JIANDAENI MATOKEO YA BRN HAYA HAPA
---
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA
WAZIRI MKUU - TAMISEMI
Uchaguzi wa wanafunzi wa kuingia Kidato
cha Tano katika shule za Serikali na Vyuo vya Ufundi kwa mwaka 2014
umekamilika. Uchaguzi umefanyika kwa kuzingatia takwimu za matokeo ya
watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne Tanzania Bara mwaka 2013.
2.0 WATAHINIWA
WALIOFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE, MWAKA 2013
Jumla
ya watahiniwa 427,679 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne
2013, wakiwemo wasichana 199,123 sawa
na asilimia 46.56 na wavulana 228,556 sawa na asilimia 53.44. Kati
yao watahiniwa 404,083 sawa na asilimia 94.48 walifanya mtihani na
watahiniwa 23,596 sawa na asilimia 5.52 hawakufanya mtihani huo.
2.1
Watahiniwa wa Shule (School Candidates)
Kwa Watahiniwa wa Shule, watahiniwa 367,163
walisajiliwa kufanya mithanikati yao wavulana ni 198,099 na wasichana ni 169,064.
ambapo watahiniwa 352,614 sawa
na asilimia 96.04 walifanya
mtihani; kati yao wasichana walikuwa 162,412 sawa na asilimia 96.07 na wavulana 190,202
sawa na asilimia 96.01. Watahiniwa 14,549 sawa na asilimia 3.96 hawakufanya
mtihani kwa sababu mbalimbali.
2.2
Watahiniwa wa Kujitegemea (Private Candidates)
Kati ya watahiniwa 60,516 wa kujitegemea waliosajiliwa kufanya mtihani, watahiniwa 51,469
sawa na asilimia 85.05 walifanya mtihani na watahiniwa 9,047 sawa na asilimia 14.95 hawakufanya
mtihani kwa sababu mbalimbali.
3.0 HALI YA UFAULU
Jumla ya watahiniwa 235,227 sawa na
asilimia 58.21 ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2013
walifaulu. Mwaka 2012 watahiniwa waliofaulu walikuwa 185,940 kati ya 431,650 waliofanya mitihani;
hii ni sawa na asilimia 43.08. Matokeo haya yanaonesha kuwa mwaka 2013 ufaulu umeongezeka kwa asilimia 15.13.
3.1 Ufaulu wa Watahiniwa wa Shule
Mwaka 2013 Watahiniwa
wa Shule waliofaulu ni 201,152 sawa na asilimia 57.05 ya
watahiniwa 352,614 waliofanya mtihani. Kwa mwaka 2013 kuna ongezeko la ufaulu wa
watahiniwa 41,405, sawa na asilimia 25.91 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka
2012 ambapo watahiniwa 159,747 walifaulu.
3.2
Ufaulu wa Watahiniwa wa
Kujitegemea
Takwimu
zimeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa watahiniwa wa kujitegemea
kutoka 26,193, sawa na asilimia 43.07 mwaka 2012 hadi kufikia
watahiniwa 34,075, sawa na asilimia 66.21 kwa mwaka 2013; Kwa kulinganisha na mwaka 2012 lipo ongezeko la asilimia 30.09
kwa ufaulu wa watahiniwa wa kujitegemea.
4.0 UCHAMBUZI WA
UFAULU
Ufaulu
wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika madaraja ya I -III umefikia
watahiniwa 71,527 sawa na asilimia 20.28 ya watahiniwa waliofanya mtihani
Tanzania Bara. Hivyo
kuna ongezeko la ufaulu wa asilimia 106.73
ikilinganishwa na matokeo ya ufaulu kwa mwaka 2012, kwa kuwa watahiniwa wa
shule waliofaulu katika madaraja I-III kwa mwaka huo walikuwa 34,599 sawa na asilimia 9.67 ya watahiniwa waliofanya mtihani.
5.0 TARATIBU ZA
UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO 2014.
Kulingana na utaratibu uliowekwa na
Serikali, mwanafunzi anayeomba kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari
kidato cha tano na vyuo vya Ufundi, hulazimika kujaza ‘Selform’ ambayo
ndiyo fomu rasmi ya maombi.
Kwa kutumia
fomu hiyo, mwanafunzi huchagua maombi matano
ya tahasusi (Combinations) za masomo anayotaka kusoma na shule anayotarajia
kujiunga nayo kwa kila chaguo.
Kamati ya uchaguzi humpanga mwanafunzi
katika machaguo yake ya masomo na shule kwa kuanzia na chaguo la kwanza. Kama mwanafunzi atakuwa
hana sifa katika machaguo yote aliyoomba, mwanafunzi husika hupangiwa chaguo la
somo alilofaulu zaidi na katika shule iliyopo karibu na wilaya yake ya makazi
kulingana na tahasusi na nafasi zilizopo
katika shule husika.
6.0 IDADI YA
WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHATANO
Jumla ya Wanafunzi 54,085 sawa na asilimia 75.61
ya wanafunzi 71,527 waliostahili
kuingia Kidato cha Tano Tanzania Bara kwa mwaka 2014 wamechaguliwa; hilo ni
ongezeko la wanafunzi 20,402 kwa
kulinganisha na wanafunzi 33,683 waliochaguliwa mwaka 2013. Kati
ya wanafunzi waliochaguliwa 2014 wavulana ni 31,352 na wasichana ni 22,733.
Wanafunzi wamechaguliwa kujiunga kidato
cha Tano katika jumla ya shule 241
zikiwemo shule 33 zilizopangiwa
wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka 2014.
Nawashukuru sana wadau wote wa elimu
katika Halmashauri mbalimbali kwa kuimarisha miundombinu ya shule hizo, ikiwemo
maabara.
Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na
kidato cha Tano 2014 ni kutoka shule za serikali na zisizo za serikali. Kati
yao wavulana 14,826 sawa na asilimia 27.41 wamechaguliwa
kusoma masomo ya sayansi na wavulana 16,526 sawa na
asilimia 30.56 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi ya Jamii. Aidha,
wasichana 7,859 sawa na
asilimia 14.53 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na wasichana 14,874 sawa na asilimia 27.50
wamepangwa kusoma masomo ya Sayansi ya Jamii.
Nawapongeza walimu wote kwa juhudi
walizozifanya katika ufundishaji kwa kuzingatia mbinu za ufundishaji walizopata
kupitia mpango wa mafunzo kazini (INSET)
kwa walimu wa sayansi na lugha (Kiswahili na Kiingereza) unaosimamiwa na Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa.
Aidha nawapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano na
Vyuo vya Ufundi.
Hali hiyo inaonesha kuwa jitihada za Serikali za kuhamasisha
vijana kusoma masomo ya Sayansi zimeanza kuzaa matunda.
Natoa wito kwa wanafunzi wa jinsi zote kujisomea
kwa bidii masomo yote, yakiwemo ya Sayansi na Sayansi
ya Jamii, kwani yanategemeana.
Walimu wa masomo ya Sayansi, Sayansi ya
Jamii na Hisabati wanakumbushwa kutumia mbinu shirikishi za kitaalam na
kisaikolojia katika kufundisha ili kuwavutia wanafunzi wengi zaidi kusoma
na kufaulu mitihani yao.
Aidha walimu wa masomo ya Sayansi, waendelee
kuwahamasisha wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi wakiwemo wanafunzi wa kike.
Aidha, wanafunzi wa kike wanapaswa kujiamini kuwa wanaweza masomo yote yakiwemo
ya Sayansi, kwani siri ya kujifunza ni utayari.
7.0 WANAFUNZI
WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA VYUO VYA UFUNDI, MWAKA 2014
Jumla ya wanafunzi 472 wakiwemo
wavulana 355 na wasichana 117 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ufundi.
Idadi ya wanafunzi hao imepungua kutoka 530 mwaka 2013 hadi 472 mwaka 2014 kwa sababu kwa sasa vyuo hivyo vimeanza
kuchukua wanachuo wa shahada ya kwanza.
Aidha, kutokana na ufaulu kuongezeka
idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na vyuo hivyo
imeongezeka kutoka wanafunzi 114
mwaka 2013 hadi wanafunzi 117 mwaka 2014 sawa na ongezeko la
asilimia 2.63.
Natoa wito kwa wanafunzi kuendelea kusoma
kwa bidii masomo ya sayansi ili mwakani idadi ya wanafunzi wanaojiunga na
mafunzo ya ufundi iongezeke ili Taifa lipate wataalam wa kutosha wa ngazi zote.
8.0 SABABU ZA WANAFUNZI KUKOSA KUCHAGULIWA
KUINGIA KIDATO CHA TANO
Jumla ya wanafunzi 16,800 wakiwemo watahiniwa wa kujitegemea 10 waliokuwa
na sifa za msingi hawakuchaguliwa kwa sababu mbalimbali zikiwemo: ufinyu wa
nafasi za shule za Kidato cha Tano (wanafunzi 16,400) na kukosa tahasusi -
Combination (wanafunzi 400).
Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa
awamu ya pili baada ya kubaini nafasi zitakazokuwa wazi zinazotokana na
wanafunzi ambao hawakuripoti awamu ya kwanza. Aidha, Serikali imeweka utaratibu
wa kuwapatia nafasi ya kusoma kidato cha Tano na cha Sita kwa pamoja na shahada
ya Ualimu wanafunzi wenye sifa.
9.0 MAMBO YA KUZINGATIA
Shule za Kidato cha Tano na Sita
zinatakiwa kuwa na mahitaji ya msingi, ikiwemo miundombinu yenye uwiano
sahihi wa vyoo, bafu, vyumba vya madarasa, bweni, jiko, bwalo, maktaba,
maabara, chumba cha Jiografia; pamoja na samani kulingana na idadi
ya wanafunzi.
Shule zenye Kidato cha Kwanza mpaka
cha Nne ambazo zinahitaji kuanzisha kidato cha Tano, zinatakiwa kuwa na miundombinu
na mahitaji kamilifu yanayotosheleza kidato cha Kwanza hadi cha Nne kabla ya
kuanza kujenga miundombinu ya Kidato cha Tano na Sita.
Natoa wito kwa Makatibu Tawala Mikoa
wawaelekeze Wakurugenzi wa Halmashauri, Miji na Majiji kuhakikisha azma ya
Serikali ya kila Tarafa kuwa na shule ya Kidato cha Tano inatekelezwa ili
kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokosa nafasi. Kutokana na ongezeko la ufaulu
wa masomo ya sayansi tunahimiza shule zitakazoanza Kidato cha Tano ziwe na
maabara ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa tahasusi za sayansi.
Aidha, shule ambazo hazikupangiwa
wanafunzi kutokana na mapungufu mbalimbali, Makatibu Tawala wa Mikoa husika
wanahimizwa kuwaelekeza Wakurugenzi kusimamia kwa karibu ukamilishwaji wa shule
hizo ili ziweze kupokea wanafunzi wa chaguo la pili (Second selection).
Natumia nafasi hii kuwahimiza wadau wote
wa Elimu kuhakikisha kuwa shule zote zinazoanzishwa kwa ajili ya kidato cha
Tano ziwe za bweni kwa kuwa wanafunzi wa kutwa ni wachache na ni lazima watoke eneo husika. Kwa mfano,
mwaka huu shule ya sekondari Buswelu ya mjini Mwanza imekosa wanafunzi kwa kuwa
ni ya kutwa na Mwanza kuna shule 3 za kutwa. Hivyo ilikuwa vigumu kupata
wanafunzi wa eneo hilo wa kutosheleza shule hizo.
Wakuu wa Shule wahakikishe kuwa wanafunzi wa kidato cha
nne wote wanajaza ‘Selforms’ kwa umakini na kwa usahihi ili kurahisisha zoezi
la uchaguzi. Aidha, wazazi kwa kushirikiana na walimu wawaelekeze watoto wao
kuwa na dira, kuwasaidia kusoma kwa malengo na kufanya machaguo ya tahasusi
kulingana na dira walizonazo.
10.0 WANAFUNZI KURIPOTI KATIKA SHULE
WALIZOPANGWA
Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato
cha Tano mwaka huu 2014, utaanza mwezi
Julai tarehe 10.
Wanafunzi wamepangwa katika shule zenye miundombinu na
walimu kwa masomo husika. Aidha, iwapo baadae mapungufu yatajitokeza, wakuu wa
shule wameelekezwa kutoa taarifa kwa uongozi wa Halmashauri husika kuhusu
upungufu huo.
Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na
kidato cha tano umefanyika kwa kutumia mfumo wa kompyuta kwa kuzingatia
machaguo ya wanafunzi pamoja na ufaulu hivyo hakutakuwa na mabadiliko yoyote.
Kwa nafasi hii, naagiza wanafunzi wote
kuripoti katika shule walizopangwa tarehe 10 Julai, 2014. Wanafunzi ambao
watashindwa kuripoti shuleni hadi tarehe 30
Julai, 2014 nafasi zao zitajazwa na wanafunzi ambao wamekosa nafasi.
11.0 HITIMISHO
Mwisho ninachukua nafasi hii kuwapongeza
wanafunzi waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi mwaka
2014, walimu, wazazi, Bodi za Shule, viongozi, jamii na wadau wote wa elimu kwa
jitihada za kuwaandaa wanafunzi, na kufanikiwa kuingia Kidato cha Tano.
Ushirikiano wa wadau wote unatakiwa ili kuboresha elimu hapa nchini.
Wataalam wa elimu kuanzia ngazi ya shule
wawe na utaratibu endelevu wa kuelimisha wadau katika utekelezaji wa malengo
yanayopimika. Katika utaratibu wa ”Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now)”; kila mmoja anatakiwa kuacha utendaji wa
mazoea na afanye kazi kwa malengo
na viwango, kuwa na mipango inayotekelezeka ya muda mfupi na muda
mrefu na kuwa na vipindi vya tathmini
kwa kila lengo kabla, kati na mwisho wa utekelezaji.
Ni matumaini
yangu kuwa wakuu wa shule na viongozi wote wa elimu wakizingatia
taratibu hizi, elimu inayotolewa hapa nchini itaendelea kuwa bora zaidi.
Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na Kidato cha Tano mwaka 2014 inapatikana katika tovuti zifuatazo: -
Ahsanteni kwa
kunisikiliza.
Mhe. Kassim M. Majaliwa (MB)
Naibu Waziri
Elimu
OFISI YA
WAZIRI MKUU - TAMISEMI
JUNI, 2014
No comments:
Post a Comment