MSANII LULU APATA DHAMANA LEO
Mahamaka Kuu Kanda ya
Dar es Salaam, leo asubuhi imempatia dhamana msanii wa filamu nchini, Elizabeth
Michael maarufu kama Lulu, anayetuhumiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba
baada ya kupitia vifungu vya sheria.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP)
kubadilisha mashitaka ya mwanadada huyo kutoka kesi ya mauaji hadi kuua bila
kukusudia.
Kutokana na badiliko hilo,
akishindwa kesi hiyo, Lulu hatapewa hukumu ya kunyongwa kwa kuwa
anatuhumiwa kwa kesi ya kuua bila kukusudia na kwa mujibu wa kifungu cha
sheria, anaweza kufungwa maisha au miaka kadhaa.
Lulu anakabiliwa na tuhuma za kumuua Kanumba aliyefariki dunia, Aprili 7, mwaka huu
nyumbani kwake Vatican, Sinza Dar es Salaam.
Lulu aliyecheza filamu kadhaa na marehemu Kanumba
waliyeibuka naye katika kundi la Kaole, Magomeni, anadaiwa kumsukuma Kanumba
nyumbani kwake Sinza Vatican, ambaye pia inadaiwa alikuwa mpenzi wake.
Inaelezwa baada ya tukio hilo, Lulu alikimbia nyumbani kwa
Kanumba na mdogo wa , Sethi Bosco akaenda kuchukua gari kumpeleka kaka yake
hospitali ya Muhimbili, ambako alipofika iligundulika amekwishafariki dunia.
Sethi alikaririwa akisema kwamba siku ya tukio, Lulu
alikwenda kwao usiku wa manane na alipofika yeye (Sethi) alimuacha aongee na
kaka yake. Sethi alidai aliwaacha sebuleni akaingia chumbani kwake na baadaye
akasikia wameingia chumbani (kwa Kanumba).
Sethi alisema baada ya muda alisikia kelele za dalili ya
ugomvi na baada ya muda Lulu alitoka kumwambia (Sethi) juu ya hali ya Kanumba
kubadilika na kuwa mbaya.
Sethi alidai aliposikia hivyo akashituka na kwenda chumbani
ambako alimkuta kaka yake katika hali mbaya, povu likimtoka mdomoni hivyo
kuchukua hatua ya kumuita daktari wake, kabla ya kumkimbiza Muhimbili.
Lulu alikamatwa asubuhi ya kuamkia siku ya tukio hilo,
linalodaiwa kutokea usiku wa manane na kuwekwa kizuizini katika kituo cha
Polisi Oysterbay, Kinondoni, Dar es Salaam, kabla ya kufikishwa mahakamani.
Uchunguzi wa madaktari katika hospitali ya Rufaa ya
Muhimbili ulisema pombe kali aina ya Jackie Daniels ilisababisha kifo cha
mwigizaji huyo.
No comments:
Post a Comment