Mbunge wa Jimbo la Ubungo -Chadema John Mnyika
---
Katika kipindi cha Hot Mix cha EATV muda mfupi uliopita Waziri wa Fedha
amesema kwamba mawazo ya kutoza elfu moja kwa mwezi kwenye kila laini ya
simu ni ya wabunge.
Kauli inayokaribiana na hiyo imewahi kuandikwa pia na Naibu Waziri wa
Wizara yenye dhamana na sekta mawasiliano kwenye mitandao ya kijamii
katika siku za karibuni. Baadaye alifuata Naibu Waziri wa Wizara ya
Fedha na sasa waziri mwenyewe. Mwaka 2012 nilitahadharisha kuhusu
udhaifu wa Rais (na Serikali) na uzembe wa Bunge katika masuala
yanayohusu maandalizi ya bajeti, hususan kutozingatiwa kwa mpango wa
taifa wa maendeleo na ongezeko la mara kwa mara la gharama za maisha kwa
wananchi. Kwa kauli hizi za Serikali udhaifu na uzembe huo unaendelea
kujihidhirisha.
Kauli hizi za Serikali ni za kujivua mzigo wa lawama baada ya malalamiko
ya wananchi kuhusu kodi hii na nyinginezo kwa kuhamisha mzigo huo kwa
wabunge.
Ni muhimu badala ya kutoa kauli za ujumla za kulaumu wabunge, Serikali
ijitokeze itaje kwa majina na wabunge gani hasa walitoa mawazo hayo.
Mimi sijawahi kutoa wazo hilo wala kuliridhia. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kwenye Hotuba yake juu ya Muswada wa Sheria ya Fedha ilipinga
pendekezo hilo lililokuwepo katika jedwali la marekebisho
lililowasilishwa na Wizara ya Fedha. Katika kuhakikisha kwamba kifungu
hicho hakipitishwi, niliwasilisha jedwali la marekebisho ya sheria
kutaka kifungu hicho kiondolewe katika muswada wa sheria ya fedha na
marekebisho yake yaliyowasilishwa na Serikali.
Hata kama ikiwa ni ukweli kwamba wazo hilo ni la baadhi ya Wabunge
(ambao ni muhimu wakatajwa kwa majina), Serikali inayokwepa kutetea
maamuzi ambayo Serikali yenyewe imeyaunga mkono inadhihirisha kwamba
imechoka na imepoteza uhalali kwa kimaadili kwa kushindwa kukubalika
mbele ya wananchi wake yenyewe (illegitimate government) .
Mamlaka na madaraka ya Bunge kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 ni
kuishauri na kuisimamia Serikali. Katika kutekeleza mamlaka hayo, Bunge
ni chombo cha uwakilishi wa wananchi na chenye mamlaka pia ya kutunga
sheria na kupitisha bajeti ya nchi. Hata hivyo, ibara ya 99 ya Katiba
imeweka mipaka kwa mamlaka hayo ya Bunge inapokuja suala la kutunga
sheria ya fedha kama hii iliyoongeza mzigo wa kodi kwa wananchi. Mamlaka
hayo yamewekwa kwa kiwango kikubwa mikononi mwa Rais kupitia Waziri
wake mwenye dhamana.
Ninachofahamu mimi ni kwamba kodi hiyo ya simu iliingizwa kwa mara ya
kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge na Rais kupitia kwa Waziri wa Fedha
aliposoma bajeti ya Serikali. Ilikuwepo kwenye Hotuba ya maandishi ya
Waziri lakini wakati wa kusoma akaruka sehemu hiyo na kutangaza kwamba
imefutwa.
Waziri wa Fedha aeleze katika hatua hiyo, wazo hilo lilitoka kwa nani
mpaka likaingia katika kitabu cha hotuba yake na nini maamuzi ya Baraza
la Mawaziri kwenye kikao kilichofanyika siku moja kabla ya yeye kusoma
hotuba yake kilichojadili hatua za kikodi (tax measures).
Kifungu hiki kilirejeshwa kwa mara nyingine tena kwenye Muswada wa
Sheria ya Fedha kupitia jedwali la Marekebisho lililowasilishwa na
Waziri wa Fedha mwenyewe. Hivyo, ajitokeze na kueleza katika hatua hiyo,
ni wabunge gani waliotaka kodi hiyo iingizwe katika muswada huo na
sababu za Wizara ya Fedha kukubaliana nao.
Uzembe wa Bunge usitumike kama kisingizio cha kuficha udhaifu wa
Serikali katika suala hili na mengine. Ni wazi, kuna uzembe pia kwa
upande wa Bunge kwa kuacha mapendekezo ya wabunge wachache yageuzwe
kinyemela kuwa ni msimamo wa wabunge wote bila ya kuwa na azimio la
Bunge kuhusu mapendekezo hayo.
Katika mchango wangu bungeni kuhusu muswada huo, nilifanya rejea ya
inayoitwa Kamati Ndogo ya Spika ya kupanua wigo wa mapato iliyoundwa
kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Bajeti; zote mbili zikiongozwa na Mh.
Andrew Chenge (Mb).
Kamati hii ambayo haijawahi kuwasilisha ripoti yake Bungeni bali kwa
Spika mwenyewe na hatimaye sasa ripoti kuwekwa kwenye maktaba ya Bunge,
bila ya ripoti hiyo kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni kama taarifa ya
kamati au walau kuwekwa mezani kama hati rasmi ya Bunge; sasa inatumika
kusukuma mzigo wa lawama kwa Bunge na wabunge.
Baada ya kamati hii, majadiliano kati ya Serikali na Kamati ya Bajeti
yaliyofanyika kwa nyakati mbalimbali yanatumika kuhalalisha maamuzi ya
Serikali yenye kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi katika
hali yenye kudhihirisha uzembe wa Bunge wa kuachia mamlaka na madaraka
yake kutumiwa visivyo.
Katika muktadha huu, kulaumiana kati ya Serikali na Wabunge au
kulalamika kwa wananchi pekee hakutoshelezi kuwezesha uwajibikaji au
mabadiliko yanayokusudiwa. Lawama ziendelee kwa kuwa zinasaidia
kuendeleza mjadala na kufanya ukweli uoendelee kutolewa na pande zote.
Malalamiko ya wananchi yaendelee kwa kuwa inawezesha Serikali na wabunge
kutambua athari za maamuzi hayo kwa wananchi.
Tunapaswa kwenda mbele zaidi kwa wewe, mimi na mwingine kuchukua
hatua? Wewe unapendekeza hatua gani zichukuliwe? Nitatoa msimamo wangu
kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa baada ya kupata maoni yenu kwa
kuniandikia kupitia mbungeubungo@gmail.com. Maslahi ya umma kwanza.
John Mnyika (Mb)
11.7.2013
No comments:
Post a Comment