Basi
la kampuni ya Mtei Express T.742 ACU linavyoonekana baada ya kuchomwa
moto na wananchi wenye hasira kali wa kitongoji cha Ijanuka kijiji cha
Kisasida manispaa ya Singida,kutokana na kugonga pikipiki aina ya Skygo
namba T.368 BXZ na kuua abiria watatu waliokuwa kwenye pikipiki
hiyo.Basi hilo lilikuwa likitoka Singida kuelekea Arusha leo
.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathanie Limu wa MOblog, Singida
WATU
watatu wa familia moja wamefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa
wakisafiria kugongwa na kuburutwa na basi la kampuni ya Mtei Express ya
mjini Arusha.
Watu
hao ni Tamili Shaban na Kassimu wamefariki dunia papo hapo kwenye eneo
la tukio ambalo ni kitongoji cha Ijanuka kijiji cha Kisasida Manispaa ya
Singida.Hamza amefariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu katika
hospitali ya mkoa mjini Singida.Miili ya watu hao imehifadhiwa katika
chumba cha mochwari katika hospitali ya mkoa.
Baba
mzazi wa watoto hao,Shaban Bunku ambaye imedaiwa ni mlinzi wa kampuni ya
TTCL mjini hapa,amelazwa katika hospitali ya mkoa na hali yake ni
mbaya.Inadaiwa kuvunjika mguu wa kulia na damu zilikuwa zikimtoka
kichwani.
Wanafamilia hao wanadaiwa walikuwa wakienda shamba kuendelea na palizi.
Akizungumzia
tukio hilo la kusikitisha,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,SACP
Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea leo saa moja na dakika moja
asubuhi huko katika kitongoji cha Ijanuka kijiji cha Kisasida.
Amesema
siku ya tukio,basi la kampuni ya Mtei lenye namba za usajili T.742 ACU
aina ya scania likiendeshwa na Dismas Ludovick,lilikuwa linatokea
Singida mjini likielekea Arusha mjini.
Kamwela
amesema lilipofika kitongoji cha Ijanuka,kwa pikipiki aina ya sky go
T.368 BXZ iliyokuwa inaendeshwa na Shaban Bunku huku akiwa amepakia
watoto wake wa kiume watatu,ilikatisha ghafla kitendo kilichosababisha
kugongwa na kuburutwa zaidi ya hatua 20.
“Dereva
wa basi hilo ambalo lilikuwa na abiria tisa,alilazimika kusimamisha
basi hilo kutokana na kuburuta pikipiki hiyo.Baada ya kusimamisha basi
hilo,wananchi wa eneo hilo walipigiana simu na ghafla walijaa na kuanza
kuvunja vunja vyoo na kisha kilichoma moto”,amesema Kamwela.
Wakati
huo huo,Kamanda Kamwela amesema wameanzisha msako mkali wa kusaka
wananchi waliojichukulia sheria mkononi ili kuwakamata waweze kufikishwa
kwenye vyombo vya sheria.
“Tabia
hii ya kujichukulia sheria mkononi haikubaliki,tutahakikisha
tumewakamata wote waliohusika na uharibifu huu.Sheria ipo wazi kwamba
hata kama mtu kafanya kosa,wananchi hawaruhusiwi kabisa kujichukulia
sheria mkononi”,alifafanua.
No comments:
Post a Comment