Muonekano wa daraja Kituo cha mabasi Ubungo jijini Dar. |
KAMPUNI ya ujenzi ya Strabag inayojenga barabara
ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) imetangaza mabadiliko ya muda
katika eneo la Ubungo jijini Dar es salaam kuanzia kesho na kesho kutwa
usiku kutokana na ujenzi unaoendelea wa barabara.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,
Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Bwana Yahya Mkumba, alisema kazi hiyo
itahusu ujenzi katika makutano ya barabara za Morogoro, Sam
Nujoma na Nelson Mandela katika eneo la Ubungo.
Alisema ujenzi huo utakaoanza leo utasababisha kufungwa kwa baadhi
ya njia katika barabara hizo kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi
keshokutwa Jumamosi.
Akielezea zaidi alisema katika awamu ya kwanza ujenzi huo
utahusisha eneo la upande wa kulia la makutano la barabara ya Sam Nujoma
na Morogoro ambalo litafungwa.
“Hali hii itasababisha magari yanayotoka maeneo ya Buguruni na
Tabata kuelekea maeneo ya Mwenge kutoweza kutumia njia ya Sam Nujoma
watakapofika taa za Ubungo,” alisema.
Alifafanua kuwa magari hayo yatalazimika kufuata alama
zitakazowaelekeza kupita katika barabara za mradi zinazojengwa hadi
barabara ya Shekilango ambapo wataweza kukutana tena na Sam Nujoma kwa
kutumia barabara ya Igesa.
Pia magari yatakayokuwa yanatokea Sinza kupitia barabara ya
Igesa hayataweza kuelekea eneo la Ubungo yatakapofika katika makutano ya
barabara za Igesa na Sam Nujoma.
Alifafanua kuwa magari yanayotumia barabara ya Morogoro
kutokea maeneo ya Mbezi na Kimara yatalazimika kuchepuka kulia na
kutumia barabara za mabasi ya mwendo wa haraka yatakapofika eneo la Kibo
ambapo patakuwa na kizuizi.
Bw. Mkumba alisema katika awamu ya pili ya ujenzi huo, eneo la
upande wa kushoto la makutano ya barabara za Morogoro na Nelson Mandela
litafungwa siku ya Jumamosi kuanzia saa nne usiku hadi saa 12 asubuhi
siku ya Jumapili.
Katika awamu hii, alisema, watumia magari yatakayokuwa
yanatokea eneo la Mwenge kutumia barabara ya Sam Nujoma yatalazimika
kuchepuka kushoto kukamata barabara ya Igesa kisha Shekilango.
Pia magari yatakayokuwa yanatokea barabara ya Nelson Mandela
na kutaka kuelekea mjini kwa kutumia njia ya Morogoro yatalazimika
kuchepuka kushoto na kwenda kugeukia eneo la Kibo ili kuikamata barabara
ya Morogoro.
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaotokea,” alisema
Bwana Mkumba na kuongeza kuwa pamoja tunajenga na hivyo usumbufu utakuwa
ni wa muda mfupi.
Mradi wa Mabasi yaendayo haraka unatarajiwa kuondoa adha ya foleni katika jiji hilo na kuleta ufanisi wa usafiri.
Ubungo Tabata Diversion
No comments:
Post a Comment