Tanzania
imetajwa kuwa nchi iliyofanikiwa kuwa na mifumo bora ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayolenga kuchochea ustawi wa maisha ya
wananchi hasa wanaoishi katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza
katika mahojiano maalum yaliyofanyika Jijini Mbeya leo, Mkuu wa Timu ya
Mifumo ya Mawasiliano wa Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta za Umma
(PS3) Bw. Desderi Wengaa, amesema kuwa hivi sasa Tanzania ni nchi ya
kupigiwa mfano kwa kuwa na mifumo bora na inayoongea, hali inayosaidia
kuimarisha huduma kwa wananchi hasa wanyonge.
PS3
ni mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la
Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID). Mradi huu wa miaka mitano
unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania bara.
“Mifumo
hii inalenga kuwawezesha watoa huduma katika ngazi ya vituo vyao kama
Zahanati, Shule na Vituo vya Afya kutoa huduma kulingana na mahitaji ya
wananchi na vipaumbele vya Serikali ambavyo kimsingi vinalenga kuwaletea
wananchi maendeleo endelevu,” alisisitiza Wengaa.
Akifanua,
Bw.Wengaa amesema kuwa mfumo kama wa Epicor 10.2 utasaidia Serikali
kujua mapato na matumizi ya fedha za umma katika sekta za kipaumbele
kama Afya na Elimu, ikiwa ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa
rasilimali zote, ikiwemo fedha zinatumika kuboresha maisha ya wananchi.
Ameongeza
kuwa kwa kutumia mifumo hiyo, thamani halisi ya fedha zitakazotumika
katika miradi ya maendeleo itaonekana na pia itaongeza muda wa
kuwahudumia wananchi katika vituo vya kutolea huduma, kwakuwa muda
utakaotumika kwa kila anayehitaji huduma kuwa mchache.
Akieleza
mikakati ya kufanya mifumo hiyo ilete matokeo tarajiwa, Bw. Wengaa
amesema kuwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) kwa kushirikiana na PS3 watakuwa na dawati la kufuatilia na
kuhakikisha kuwa mifumo yoye inafanya kazi na kuleta matokeo tarajiwa.
Akizungumzia
moja ya mfumo unaotumika katika sekta ya afya (Government of Tanzania
Hosipital Management System – GoT-HoMIS) amebainisha kuwa unasaidia
kutunza kumbukumbu za mgonjwa kuanzia siku ya kwanza anapofika kupata
huduma, hivyo kuisaidia Serikali katika kutambua mahitaji halisi katika
maeneo husika na hivyo kuboreshwa kwa huduma zinazotolewa.
Wakati
Mfumo mwingine ni ule unaotumika katika kupanga mipango, bajeti na
kutoa taarifa (PlanRep) ambao unasaidia watendaji katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa kuandaa mipango na bajeti katika vituo vyao na
kuiwasilisha Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kupitia mfumo huo, hivyo kuokoa
rasilimali fedha na muda uliokuwa unatumika awali kuandaa mipango na
bajeti hizo.
Tanzania
kutajwa kuwa nchi ya kupigiwa mfano ni kutokana na pia kuwepo kwa
mifumo kama ile ya kubaini mahitaji ya watumishi katika sekta ya afya,
hasa katika vituo vya kutolea huduma na vipaumbele vya eneo husika.
Kuhusu
mifumo hiyo kuongea, Wengaa amebainisha kuwa, hali hiyo itasaidia
kubainisha uwiano wa majukumu kati ya mtumishi mmoja na mwingine katika
vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo kubaini watumishi wanatekeleza
majukumu mengi zaidi kuliko inavyotakiwa ili kuweza kuongeza watumishi
wengine katika eneo hilo.
Baadhi
ya mifumo hiyo ni PlanRep, WISN na POA, GoT-HoMIS na mfumo wa kuandaa
taarifa za uhasibu katika ngazi ya kutolea huduma (FFARS), ambayo iko
chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. WISN na
POA inasimamiwa kwa pamoja na Ofisi ya Rais Utumishi, ikiwa ni moja ya
hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo
kuboresha huduma za afya hapa nchini.
Mkuu
wa Timu ya Mifumo ya Mawasiliano wa Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta
za Umma (PS3) Bw. Desderi Wengaa akisisitiza kuhusu umuhimu wa mifumo
hiyo katika kuwaletea wananchi maendeleo, wakati wa mahojiano maalum leo
Jijini Mbeya
No comments:
Post a Comment