
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Mh James Mbatia wa Nccr-Mageuzi
---
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amezindua Tume maalum aliyoiunda ili ifanye uchunguzi wa matokeo ya
mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na
kuwataka wajumbe wa Tume hiyo watafute kiini cha mserereko wa kushuka
kwa ufaulu kuanzia mwaka 2010 hadi 2012.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi
(Jumamosi, Machi 2, 2013) wakati akizungumza na wajumbe wa Tume hiyo
kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Dk. Shukuru Kawambwa.
“Nimetafuta takwimu za tangu
mwaka 2005, Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani na kubaini
kuwa tangu wakati huo hadi mwaka 2009 tulikuwa tukifanya vizuri, lakini
kuanzia mwaka 2010 hadi 2012 matokeo yamekuwa yakishuka sana,”
aliwaambia wajumbe wa Tume hiyo na waandishi wa habari waliohudhuria
uzinduzi huo.
Alisema hali hiyo haikuwa kwenye
shule za sekondari za umma (kata) peke yake bali hata kwa shule za
Serikali, za watu binafsi na kwenye seminari ambazo kwa miaka mingi
zimekuwa na sifa ya kufanya vizuri kuliko shule za kawaida.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu
alisema: “Mwaka 2005 kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 89.3; mwaka
2006 asilimia 89.12; mwaka 2007 asilimia 90.6; mwaka 2008 asilimia 83.6
na mwaka 2009 asimilia 72.5, hapa napo tulikuwa bado tuko vizuri japo si
sana ikilinganishwa na miaka mine iliyotangulia.”
“Lakini mwaka 2010, kiwango cha
ufaulu kilishuka na kufikia asilimia 50.4, mwaka 2011 kilipanda kidogo
na kufikia asilimia 53.6 na kilishuka zaidi mwaka jana ambapo kilifikia
asilimia 34.5. Hapa ni lazima mtu utapata maswali ya msingi na kujiuliza
nini kimetokea katika miaka ya hivi karibuni,” alisema.
Waziri Mkuu alibainisha kwamba
idadi ya watahiniwa iliongezeka kutoka 85,292 mwaka 2005 na kufikia
248,336 katika mwaka 2009 wakati idadi ya walimu nayo pia iliongezeka
kutoka 20,414 na kufikia 37,218 katika kipindi hichohicho.
Alisema anatambua changamoto
nyingine zinazoikabili sekta ya elimu kama vile uhaba wa vitendea kazi,
upungufu wa maabara na walimu wa sayansi, upungufu wa mabweni pamoja na
nyumba za walimu.
Kinachoshangaza, Waziri Mkuu
alisema, mbali na kuongezeka kwa walimu kutoka 44,053 mwaka 2010, walimu
55,982 (mwaka 2011) na kufikia walimu 68,784 mwaka 2012 bado kiwango
cha ufaulu nacho kilikuwa kikishuka katika kipindi hichohicho.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu
alisema: “Kwenye shule za kata, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 114,883;
mwaka 2011 wanafunzi 106,286 na mwaka 2012 wanafunzi 74,817 wakati
kwenye shule za Serikali, katika kipindi hicho hicho ufaulu ulishuka
kutoka wanafunzi 19,412, na kufikia wanafunzi 10,712.”
Waziri Mkuu alisema katika
mchanganuo huo, jambo moja kuu lililo bayana ni kuwepo kwa mzao wa
kwanza wa shule za kata katika mwaka 2010 lakini bado athari za kushuka
kwa ufaulu zikasambaa kote hadi kwenye shule za serikali, za binafsi na
seminari.
Akianisha kushuka kwa ufaulu wa
daraja la kwanza katika makundi hayo, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2010,
kwenye shule za kata, walifaulu wanafunzi 1,225 wakati mwaka 2011
walikuwa wanafunzi 564 na mwaka 2012 walikuwa wanafunzi 162”.
“Kwenye shule za Serikali, mwaka
2010, walifaulu wanafunzi 952, mwaka 2011 wanafunzi 771 na mwaka 2012
wanafunzi 253. Kwenye shule za binafsi, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi
2,476 mwaka 2011 wanafunzi 1,614 na mwaka 2012 wanafunzi 1,032. Kwenye
seminari, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 695, mwaka 2011 wanafunzi 428
na mwaka 2012 wanafunzi 197.”
Akianisha matokeo ya waliofeli
kwa kupata daraja ‘0’, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2010, kwenye shule za
kata, walifeli wanafunzi 151,848 wakati mwaka 2011 walifeli wanafunzi
143,552 na mwaka 2012 walifeli wanafunzi 223,774”.
“Kwenye shule za Serikali, mwaka
2010, walifeli wanafunzi 7,926, mwaka 2011 wanafunzi 9,790 na mwaka
2012 wanafunzi 16,176. Kwenye shule za binafsi, mwaka 2010, walifeli
wanafunzi 13,346 mwaka 2011 wanafunzi 16,620 na mwaka 2012 wanafunzi
25,055. Kwenye seminari, mwaka 2010, walifeli wanafunzi 638, mwaka 2011
wanafunzi 972 na mwaka 2012 wanafunzi 1,329.”
Alisema kwa mujibu wa hadidu za
rejea, wajumbe wa tume hiyo watatakiwa kuangalia ni sababu zipi
zimechangia kuwepo kwa matokeo hayo mabaya, mserereko wa kushuka umekuwa
ukiongezeka kwa sababu gani, usimamizi katika Halmashauri ukoje,
ukaguzi wa elimu na uhamishiwaji wa sekta ya elimu kwenye Wizara ya
TAMISEMi umechangiaje kushuka kwa kiwango cha ufaulu.
Vilevile, watatakiwa kuangalia
mitaala na mihutasari ikoje, kuangalia uwiano uliopo kwenye mitihani
inayotungwa ikiwa ni pamoja na uhakiki wa mitihani hiyo; kuangalia
mazingira ya kufundishia, mfumo wa upimaji, usimamizi na uendeshaji, na
kutokuwepo kwa chakula shuleni kunachangiaje kushuka kwa utendaji mbaya
wa wanafunzi katika masomo yao.
Tume hiyo yenye wajumbe 15,
imepewa muda wa wiki sita kuanzia Machi mosi iwe imekamilisha kazi hiyo
na kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri Mkuu. Itaongozwa na Prof. Sifuni
Mchome wa Tume ya Vyuo Vikuu, na Makamu wake atakuwa Bi. Bernadetha
Mushashu (Mbunge wa Viti Maalum – Kagera).
Wajumbe wengine ni Bw. James
Mbatia (mbunge wa Kuteuliwa), Bw. Abdul J. Marombwa (Mbunge wa Kibiti),
Prof. Mwajabu Possi (Chuo Kikuu – UDSM), Bibi Honoratha Chitanda (CWT)
na Bibi Daina Matemu (TAHOSSA) na Bw. Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).
Wengine ni Bw. Rakhesh Rajani
(TWAWEZA), Bw. Peter Maduki (CSSC), Mwl. Nurdin Mohamed (BAKWATA), Bw.
Suleiman Hemed Khamis (Baraza la Wawakilishi), Bw. Abdalla Hemed Mohamed
(Chuo Kikuu – SUZA), Bw. Mabrouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Z’bar na
Bw. Kizito Lawa (Taasisi ya Kukuza Mitaala)
No comments:
Post a Comment