airtel
.
Wednesday, January 9, 2013
JK; SERIKALI ITAAJIRI WALIMU WENGI MWAKA HUU 2013
Mpaka sasa, Tanzania ina upungufu wa walimu 57,177 katika shule za Serikali, tatizo ambalo Serikali inasema italimaliza katika miaka michache ijayo, kutokana na idadi kubwa ya walimu wanaofundishwa katika vyuo mbalimbali kuhitimu masomo.
Rais Jakaya Kikwete, alitoa kauli hiyo mjini Igunga juzi, ambapo alisema kati ya walimu watakaoajiriwa na kusambazwa, 14,600 watakuwa wa shule za msingi, walimu 14,060 watakuwa wa shule za sekondari na 80 watakuwa walimu wa vyuo vya ualimu.
Akihutubia maelfu ya wananchi wa mjini Igunga kwenye Uwanja wa Barafu, Rais Kikwete alisema mikoa yenye uhaba mkubwa zaidi wa walimu, ndiyo itapewa kipaumbele katika mgawo huo wa walimu.
Mkoa wa Tabora ni moja ya mikoa yenye uhaba mkubwa wa walimu, ikiwa na ukosefu wa walimu 2, 055 na Wilaya ya Igunga pekee inahitaji walimu 285.
Hii itakuwa mara ya pili, Serikali kuajiri na kusambaza idadi kubwa ya walimu wa shule za msingi na sekondari katika jitihada za kumaliza tatizo hilo.
Mwaka juzi, Serikali iliajiri na kusambaza walimu 24,621 ambao kati yao 11,379, walikuwa wa shule za msingi, walimu 13,246, walikuwa wa shule za sekondari na walimu 42 walikuwa ni wa vyuo vya elimu.
Wakati shule za Serikali, zinaendelea kukabiliwa na upungufu wa walimu, shule binafsi zina ziada ya walimu, shule za msingi zikiwa na ziada ya walimu 2, 857 na zile za sekondari zikiwa na ziada ya walimu 459, hali inajionyesha katika matokeo mazuri ya mitihani kwa wanafunzi wa shule hizo.
Rais Kikwete aliwaambia wananchi kuwa Serikali, inakabiliana ipasavyo na matatizo mengine yanayoikabili sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara, ukosefu wa nyumba za kutosha za walimu na ukosefu wa vitabu vya wanafunzi.
Pia alizungumzia suala la huduma ya maji, akisema Serikali imeonyesha jitihada za kukabiliana na ukosefu wa maji katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Kwa upande wa Igunga, Rais Kikwete alisema kufuatia kuzinduliwa kwa mradi wa Maji wa Bulenya, mji wa Igunga na vijiji vitatu vinavyozunguka mji huo sasa vinapata maji kwa asilimia 70.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment