Na Veronica Kazimoto – MAELEZO
Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe. Philipo Mulugo
ametangaza matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Elimu ya Sekondari Kidato cha
Pili mwaka 2012, ambapo kiwango cha ufaulu kimepanda kutoka asilimia
45.40 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 64.55 mwaka 2012.
Matokeo hayo yametangazwa mbele ya waandishi wa habari leo
jijini Dar es Salaam ambapo idadi ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya
mtihani walikuwa 430,327, kati yao wasichana walikuwa 205,476 na
wavulana 224,851, ikiwa ni upungufu wa watahiniwa 36,240 ikilinganishwa
na mwaka 2011 ambao walikuwa 466,567.
“Watahiniwa 386,271 sawa na asilimia 89.76 ya waliosajiliwa,
walifanya mtihani wakiwemo wasichana 187,244 na wavulana 199,027,
watahiniwa 44,056 sawa na asilimia 10.24 hawakufanya mtihani, kati yao
wasichana ni 18,231 na wavulana 25,825” amesema Mulugo.
Aidha Waziri Mulugo amefafanua kuwa watahiniwa 136,946 ambao
wameshindwa kupata wastani wa ufaulu wa alama 30 na wale waliofutiwa
matokeo yao kutokana na udanganyifu watalazimika kukariri kidato cha
pili mwaka 2013.
“Ni vema ikaeleweka kuwa kukariri kidato si adhabu bali ni
kutoa fursa nyingine kwa mwanafunzi kuweza kupata maarifa, stadi na
ujuzi wa elimu ya sekondari, hivyo ni matumaini yangu kuwa wanafunzi
hawa watafanya bidii katika kujifunza na kuzingatia masomo ili waweze
kufaulu masomo yao katika kiwango kinachotakiwa” amesisitiza Mulugo.
Mtihani wa Taifa wa Elimu ya Sekondari Kidato cha Pili
ulifanyika nchini kote kuanzia tarehe 05 Novemba, 2012 na kumalizika
tarehe 16 Novemba, 2012 kukiwa na jumla ya vituo 4,304 vilivyosajili
watahiniwa, sawa na ongezeko la vituo 117 ikilinganishwa na ile ya mwaka
2011
No comments:
Post a Comment